– Mti Wenye Mchanganyiko Wa Viungo Vyote,
Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: KIUNGO cha chakula kijulikanacho kama ‘Allspice’ kimekuwa kivutio kwa wananchi wanaofika katika Banda la Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), lililopo katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yajulikanayo kama Sabasaba yanayoendelea mkoani Dar es Salaam.

Mtafiti kutoka TARI Kituo cha Mlingano Tanga, Dkt, Mgaya Maumba amesema kwamba kwenye maonesho hayo wamekwenda na miche ya viungo ikiwemo iliki, mdalasini na mche huo wa ‘Allspice’ ambao ni kiungo ambacho sio kigeni duniani, ila kwa Tanzania ni kigeni.
“Mti huu unaitwa Allspice au mchanganyiko wa viungo vyote, ni mti ambao umekusanya kiungo zaidi ya kimoja katika harufu yake, ukinusa utasikia harufu ya karafuu, harufu ya iriki, mdalasini na viungo vingine,
“Ni mti mmoja umekusanya kiungo zaidi ya kimoja katika harufu, pia una manufaa makubwa katika matumizi ya viungo, unapikia vyakula vingi, inatumika kama kiungo cha chai, supu, biriani, hata katika ‘ Ice cream’ au sehemu ya kuokea mikate,” amesema.
Amesema kiungo hicho kina faida nyingi kiafya, pia husaidia mmeng’enyo wa chakula tumboni, kinatumika na Wajamaika wanakunywa kama chai kutibu maumivu ya kichwa, misuli na meno.
Amesema kiungo hicho pia kinasaidia kupunguza shinikizo la damu, pia kupambana na vimelea vya ukuaji wa kansa.
“Kwa hiyo wataalam wanasema kiungo hichoi kinatumika kama tiba ya kansa, tezi dume na kansa ya matiti kwa kina mama, kinazuia maumivu kwa kina mama wanapokuwa katika siku zao,” amesema.
Amesema ni kiungo kinatumika kama kinywaji lakini kina manufaa makubwa kiafya.
Amesema mtu anaweza kutumia majani ya mti wa kiungo hicho, matunda au magome yake japo wanashauri watu watumie majani kwa kuwa wakitumia magome wataua mti.