Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM: TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania ( TARI), imesema watafiti wa kilimo wanaendelea kufanya tafiti zenye majibu chanya ili kutatua changamoto zinazosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.
Mratibu Kitaifa wa Zao La Mtama kutoka TARI Ilonga – Kilosa Mkoani Morogoro, Emmanuel Mwenda amesema hayo Dar es Salaam ikiwa ni mwendelezo wa Mkutano kwa wadau wa Mazao ya Karanga, Maharage na Mtama.
Mwenda amesema kutokana na changamoto hiyo, yamesababisha mbegu zilizokuwa zikifanya vizuri zamani kupungua ufanisi na tija hivyo kama watafiti inawafanya waendelee kutafiti ili wapate majibu ya changamoto hizo.

Ametoa ufafanuzi huo alipokuwa akijibu swali la mkulima aliyetaka kujua kwanini TARI inagundua mbegu mpya wakati za zamani zipo.
Naye Meneja kituo cha TARI Mikocheni Dar es Salaam, -Dkt. Freddy Tairo amesema taasisi hiyo imegundua teknolojia mbalimbali ikiwemo mbegu bora za maharage, mtama na karanga ili kuongeza tija.
Kwa upande wake msindikaji wa siagi ya karanga, Agatha Laizer amewashauri wadau wa Kilimo kama Wakulima na wasindikaji wa bidhaa za Kilimo kutafuta taarifa mbalimbali za Kilimo kutoka kwa wataalamu wa kilimo wakiwemo TARI.
Amesema ushauri huo wa kuwawezesha kujua aina ipi ya mbegu inafaa kwa usindikaji wa siagi ili kupata tija kutokana na shughuli mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa kilimo.

Mktano huo ulianzia Arusha, Dodoma kisha Dar es Salaam, lengo ikiwa ni kutoa matokeo ya tafiti mbalimbali zilizofanyika zikilenga kubaini uhitaji wa soko na kusambaza Mbegu mpya za Mazao hayo zenye tija zaidi.