Na Lucy Ngowi
MOROGORO: MATUMIZI ya chokaa ya kilimo ni suluhishoi katika kukabiliana na changamoto za tindikali na chumvi chumvi kwenye udongo ambazo hupunguza kwa kiasi kikubwa tija ya kilimo nchini.
Mratibu wa Utafiti na Ubunifu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Mlingano Tanga. Dkt. Sibaway Mwango amesema hayo katika Maonesho ya Nanenane ya Mwaka huu 2025, Kanda ya Mashariki yanayofanyika katika Uwanja wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mkoani Morogoro.
Amesema chokaa ya kilimo inapaswa kuwekwa wakati wa maandalizi ya shamba, kabla ya kupanda au kuweka mbolea, ili kuondoa tindikali na kurekebisha usawa wa virutubisho.

Ametaja mikoa ya Nyanda za Juu Kusin ambayo ni Iringa, Njombe, Songwe, Rukwa na Katavi,
Pia mikoa ya Kusini ambayo ni Ruvuma na Mtwara, Magharibi ya Kati ambayo ni Singida, Tabora, Kigoma na Kanda ya Ziwa, Bukoba, Geita na Mara imeathirika kwa kiwango kikubwa cha tindikali,
Hali inayosababisha upotevu wa zaidi ya asilimia 50 ya mbolea inayowekwa shambani na hatimaye kusababisha upungufu mkubwa wa mavuno.
Katika Nanenane ya mwaka huu, TARI Mlingano imejikita kuhamasisha wakulima na wadau juu ya umuhimu wa kupima afya ya udongo kabla ya kilimo, kama hatua ya msingi ya kilimo chenye tija na endelevu.
Wakulima wanahimizwa kufika katika banda la TARI Mlingano wakiwa na sampuli za udongo ambapo hupimiwa bure na kupewa ushauri wa kitaalamu.
Mbali na utafiti wa udongo, TARI Mlingano ina jukumu la utafiti wa zao la mkonge, na inatarajiwa kupewa majukumu mapya ya kufanya tafiti kuhusu mazao ya jamii ya michungwa pamoja na viungo.
Katika Maonesho ya Wakulima (Nanenane) 2025, TARI kupitia Kituo cha Mlingano, imewasilisha mbinu hizo kama sehemu ya mikakati ya kulinda afya ya udongo na kuongeza mavuno kwa wakulima.
TARI Mlingano imeandaa miongozo mbalimbali kwa njia ya ramani za udongo zinazobainisha changamoto kuu za afya ya udongo, ikiwa ni pamoja na ongezeko la tindikali na chumvi chumvi katika maeneo mbalimbali ya nchi.