Yazalisha Miche Bora na Kufundisha Wakulima
Na Lucy Ngowi
MOROGORO: Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imesema licha ya kuwepo kwa teknolojia mbalimbali za kuboresha kilimo cha minazi, bado wadau wengi hawajaweza kuzijua wala kuzifikia.
Akizungumza katika Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki, Mratibu wa Uhaulishaji wa Teknolojia na Mahusiano kutoka Kituo cha TARI Mikocheni, Vidah Mahava, amesema wameanzisha mkakati maalum wa kufufua na kuendeleza kilimo cha minazi nchini kwa kutumia mbinu mbalimbali.

Hatua kubwa zilizochukuliwa na kituo hicho ni kuzalisha mbegu bora, kutoa mafunzo kwa wakulima, na kuanzisha vitalu vya miche katika maeneo mbalimbali nchini.
Hata hivyo, changamoto kubwa ni ukosefu wa taarifa na elimu sahihi kwa wakulima kuhusu teknolojia za kisasa za minazi, zikiwemo mbegu bora, kanuni za upandaji, na udhibiti wa magonjwa na wadudu waharibifu kama vile mbu wa minazi na chonga.
Baadhi ya wakulima hulima minazi bila kufuata kanuni, huku wengine wakishindwa kutambua tofauti kati ya kole lenye ugonjwa na lenye afya.
Ugonjwa wa kunyong’onyea umetajwa kuwa tishio kubwa kwa minazi, lakini wengi hawana elimu ya kuutambua na kuukabili. Ili kuhakikisha teknolojia hizi zinawafikia wananchi,
TARI kupitia Kituo cha Mikocheni kinaendelea kuzalisha miche bora ya minazi kwenye vitalu. Tayari miche imepelekwa kwa awamu mbili katika mikoa ya Lindi na Mtwara, kutokana na ombi la wananchi kwa Rais Samia Suluhu Hassan alipowatembelea.
Kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na 2024/2025, miche yote iliyozalishwa kwenye vitalu vya vituo vidogo vya TARI Mikocheni iligawiwa kwa wananchi.

Pamoja na kuzalisha miche katika vituo hivyo, juhudi zimefanyika kuanzisha vitalu vya pamoja kati ya TARI na halmashauri za mikoa inayolima minazi nchini. Vitalu hivyo vimeanzishwa katika Halmashauri za Ruangwa (Lindi), Muheza (Tanga), na Mtwara Vijijini (Mtwara).
Halmashauri hizi tatu zilipokea mbegu 6,000 kila moja, ambazo tayari ziliota na kugawiwa kwa wakulima ndani ya halmashauri zao. Aidha, TARI Mikocheni kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mkinga (Tanga) wameanzisha kitalu cha pamoja chenye mbegu 6,000 ambazo bado ziko ardhini mpaka zitakapokuwa tayari kugawiwa.
Mazungumzo yanaendelea baina ya TARI na Halmashauri ya Same (Kilimanjaro) kwa ajili ya kupeleka mbegu zaidi. Mpango wa upandaji wa minazi unafanyika kwa uwiano wa mita 10 kwa 10, ambapo ekari moja hupandwa miti 40, na kila mti una uwezo wa kutoa nazi 35 hadi 40 kwa mwaka.
Mbali na minazi, kituo hicho kinaendelea na utafiti wa maabara kwa ajili ya utambuzi wa magonjwa ya minazi na mazao mengine, pamoja na kuzalisha miche kwa kutumia teknolojia za kisasa (kwa njia ya chupa) kwa mazao kama mananasi, mihogo, viazi vitamu, na mkonge.
Mojawapo ya mafanikio mapya ni teknolojia ya uzalishaji wa mananasi aina ya MD2 kwa njia ya chupa. Mananasi haya ni bora kwa Biashara, yanafaa kwa juisi, yana ladha tamu, hayaozi haraka, na yana soko kubwa ndani na nje ya nchi iwapo uzalishaji utakuwa wa kutosha.
7Mashamba darasa ya mananasi haya yalifanyika Bagamoyo (Pwani), Kinole (Morogoro), na Madeke (Njombe).

Kupitia mafunzo kwa wakulima, vijana, wanawake, na wazee, TARI Mikocheni inalenga kuhakikisha teknolojia hizi haziishii kwenye maonesho ya kilimo, bali zinamfikia mkulima wa kawaida vijijini.