Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM: CHANGAMOTO za mabadiliko ya tabia nchi, zimesababisha mbegu zilizokuwa zikifanya vizuri zamani kupungua ufanisi na tija, jambo linalowafanya watafiti wa kilimo kuja na majibu ya changamoto hizo.
Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Emmanuel Mwenda amesema hayo katika Mkutano wa wadau wa mazao ya karanga, maharage na mtama mkoani Dar es Salaam, baada ya mkutano kama huo kufanyika Arusha na Dodoma.
Mwenda mtafiti kutoka TARI Ilonga iliyopo Kilosa Morogoro, pia ni Mratibu Kitaifa wa zao la mtama amesema hayo alipokuwa akijibu swali la Mkulima aliyetaka kujua kwanini TARI inatafiti Mbegu wakati nyingine zipo.
Naye Meneja kituo cha TARI Mikocheni- Dkt. Freddy Tairo amesema TARI imegundua Teknolojia mbalimbali ikiwemo Mbegu bora za Maharage, Mtama na Karanga ili kuongeza tija.
Amesema taasisi hiyo inaendelea kufanya utafiti wa mbegu bora ili kuendelea kugundua teknolojia bora za Kilimo zinazolenga kujibu changamoto mbalimbali zinazoibuka na kuathiri upatikanaji wa tija katika mnyororo mzima wa thamani wa Kilimo.
Miongoni mwa sababu zinazotajwa kuathiri tija ni mabadiliko ya tabia nchi ambayo huleta changamoto mpya ikiwemo magonjwa na hata magugu ambayo awali hayakuwepo.
Agatha Laizer, ambaye ni msindikaji wa siagi ya Karanga amewashauri wadau wa Kilimo kama Wakulima na wasindikaji wa bidhaa za Kilimo kutafuta taarifa mbalimbali za Kilimo kutoka kwa Wataalamu kama TARI,
Ikiwemo aina ipi ya Mbegu inafaa kwa usindikaji wa siagi ili kupata tija kutokana na shughuli mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa kilimo.