Na Lucy Ngowi
MOROGORO: TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), imefanikiwa kuboresha aina mpya za mbegu za mtama, uwele na ulezi zenye uwezo wa kustahimili mashambulizi ya ndege na kiduha (gugu chawi), ambayo ni changamoto kubwa kwa wakulima.
Mtafiti Msaidizi kutoka TARI Ilonga iliyopo Kilosa mkoani Morogoro, David Macha amesema hayo katika Maonesho ya nanenane Kanda ya Mashariki, ambayo kilele chake kilikuwa ni jana Agosti nane, 2025.

Amesema kwa upande wa mtama, wamezalisha aina tatu mpya: aina mbili nyeupe ambazo ni fupi, na aina moja nyekundu ndefu. Aina ya ‘Macia’ ni mojawapo ya mbegu nyeupe, yenye urefu wa mita 1.5, ambayo inafanya vizuri kibiashara hasa katika utengenezaji wa bia, ikichukua nafasi ya shayiri na ngano zilizokuwa zikitumika awali.
Amesema mbegu hiyo ya macia hukaa shambani kwa siku 110 na hutoa mavuno ya tani 3.8 kwa hekta moja, ikilinganishwa na mbegu za zamani zilizokuwa zikitoa tani 2.

Ina masuke makubwa na uwezo mkubwa wa kustahimili mashambulizi ya ndege kutokana na ubunifu wa kiteknolojia unaofanya isiwe ya kuvutia kwa ndege.
Ametaja mbegu nyingine mpya kuwa ni TARI SOR 1 na TARI SOR 2, ambazo zimeundwa kuzuia mashambulizi ya kiduha, adui mkubwa wa mazao ya nafaka.
Kwa upande wa uwele, amesema wamezalisha aina iitwayo Okoa, ambayo ina kiwango kikubwa cha madini ya zinki, muhimu kwa kinga na uzazi wa binadamu.
Amesema madini hayo ya Zinki ni nadra kupatikana kwa wingi kwenye nafaka nyingine, na hivyo aina hii ni suluhisho bora kwa lishe bora.
Katika zao la ulezi, amesema TARI Ilonga wamezalisha aina tatu, ikiwemo aina mpya iliyo na uwezo wa kutoa hadi kilo 1,200 kwa ekari moja, tofauti na aina ya P224 inayotoa kilo 700 na 415 inayotoa kilo 800.
Aina hiyo mpya imeboreshwa pia kukabiliana na ugonjwa wa ‘blast’ unaoshambulia masuke.
Ulezi pia umetajwa kuwa na virutubisho vingi vikiwemo kiwango kikubwa cha calcium, na hivyo kuwa muhimu kwa afya ya binadamu hasa watoto na wazee.