Na Mwandishi Wetu
TANZANIA imepata dola za Marekani bilioni 2.32 kwa kuuza tani milioni 1.57 za mazao ya matunda na jamii ya kunde nchini China, India, Marekani, Pakistan na Brazil.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hayo leo wakati akizungumza na viongozi na wananchi mbalimbali waliohudhuria ufunguzi wa Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Sherehe za Nanenane ya Mwaka 2024 katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.
Amesema Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko imeingia makubaliano ya kuuza tani milioni 1.25 za mahindi.
“Kati ya hizo, tani 650,000 zitauzwa Zambia; tani 500,000 zitauzwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na tani 100,000 kwa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali imewezesha upatikanaji wa soko la vanilla, pilipili manga, karafuu, nanasi, kakao, viazi mviringo, tumbaku na ndizi katika nchi za China, Marekani, Pakistani, Afrika Kusini na India ambayo yanatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni.
“Kwa upande wa wafugaji, hadi Aprili, 2024 jumla ya tani 13,745 za nyama zenye thamani ya dola za Marekani milioni 56 zimeuzwa katika nchi za Bahrain, Comoro, Hong Kong, Jordan, Kenya, Kuwait, Oman, Qatar, Rwanda, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Vietnam.
Pia vipande 1,542,916 vya ngozi vyenye thamani ya shilingi bilioni saba vimeuzwa katika nchi za Nigeria, Togo, Kenya, Ethiopia na Pakistan.” amesema.
Kwenye sekta ya uvuvi, Waziri Mkuu amesema hadi kufikia Aprili, 2024, tani 41,271 za mazao ya uvuvi na samaki hai wa mapambo 134,572, wenye thamani ya shilingi bilioni 515.78, waliuzwa katika nchi za Umoja wa Nchi za Ulaya, Canada, Marekani, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, China, Zambia, Uganda na Malawi.