Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, ameishukuru Serikali ya China kwa kuendeleza programu maalum zinazolenga kudumisha na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na China.
Akizungumza katika hafla ya Mashindano ya Walimu wa Lugha ya Kichina Afrika yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mtambule amesema mashindano hayo ni ishara muhimu ya kuimarika kwa ushirikiano wa kimataifa, hasa katika eneo la lugha na utamaduni.

Amesema mashindano hayo yamehusisha takribani washiriki 20 kutoka nchi mbalimbali za Afrika, wote wakiwa ni walimu wa lugha ya Kichina.

Mtambule amesema lugha ni nyenzo muhimu katika kukuza diplomasia ya uchumi na kuimarisha uhusiano wa kijamii kati ya mataifa.
Pia amefurahishwa kusikia mipango mbalimbali inayolenga Afrika Mashariki, na akaomba kituo cha mafunzo cha Afrika Mashariki kijengwe katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili kuimarisha zaidi ushirikiano huo.

Amesema ni heshima kubwa kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo kwa mara ya pili, jambo linalodhihirisha uwezo wa nchi katika kuratibu matukio ya kimataifa.
Amekumbusha kuwa katika maboresho ya hivi karibuni ya mitaala nchini, Serikali imeongeza lugha ya Kichina katika orodha ya lugha za kigeni zinazofundishwa na kutahiniwa katika ngazi mbalimbali za elimu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utafiti na Machapisho wa UDSM, Dkt. Mathew Senga, akimwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa William Anangisye, amesema tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Confucius mwaka 2013, imekuwa kiungo muhimu cha ushirikiano kati ya Tanzania na China kupitia ufundishaji, utafiti, ushauri wa kitaalamu na shughuli za kitamaduni.
Amesema Taasisi hiyo pia imekuwa daraja la kuwaunganisha vijana wa Kitanzania na fursa za ufadhili pamoja na ajira, kupitia mahusiano yake na makampuni mbalimbali ya Kichina nchini.
UDSM, kupitia programu zake nyingi za lugha ya Kichina, imeendelea kuwa kinara katika kufundisha lugha na utamaduni wa taifa hilo, huku wanafunzi wakipata nafasi ya kujifunza Kichina kama somo la hiyari.

Dkt. Senga amesena,”Nina imani kila mmoja amefika hapa kwa sababu ana uwezo. Jiulizeni barani Afrika kuna walimu wangapi wa Kichina?
“Kwanini ni ninyi pekee mmechaguliwa? Jibu ni rahisi: mnaweza. Msiwe na huzuni kwa watakaokosa nafasi ya ushindi; jaribuni tena kwa wakati mwingine.”









