Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimezindua rasmi Kituo cha Ushirikiano wa Elimu ya Kidijitali kati ya China na Afrika ikiwa ni hatua kubwa ya kuimarisha elimu ya kisasa kwa kutumia teknolojia bunifu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Taaluma na Utafiti, Profesa Nelson Boniface, amesema kuanzishwa kwa kituo hicho ni mafanikio makubwa katika safari ya mageuzi ya elimu barani Afrika.
“Ni heshima kubwa kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwa mwenyeji wa kituo hiki muhimu. Tunapitia zama za mabadiliko makubwa ya kiteknolojia, na ni wajibu wetu kuhakikisha walimu wetu wana ujuzi na uwezo wa kutumia zana za kisasa za kidijitali katika ufundishaji, hasa katika masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM),” amesema Profesa Boniface.
Amesema Kituo hicho kimeanzishwa kwa ushirikiano kati ya UDSM na Zhejiang Normal University ya China, kikilenga kukuza uwezo wa walimu na wakufunzi katika kutumia teknolojia ya kidijitali katika kufundisha na kujifunza.

Pia amesema mafunzo ya wiki moja yameandaliwa kwa walimu wa shule za msingi, sekondari, na wakufunzi wa vyuo, yakiwa na lengo la kuwawezesha kufundisha kwa mbinu bunifu na zinazokidhi mahitaji ya karne ya 21.

Profesa Boniface amekishukuru Chuo Kikuu cha Zhejiang Normal kilichopo nchini China kwa ushirikiano thabiti, pamoja na Shule ya Elimu ya UDSM na Taasisi ya Confucius kwa maandalizi ya tukio hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Elimu ya UDSM, Dkt. Nkanileka Mgonda, amesema uzinduzi wa kituo hicho ni ushahidi wa dhamira ya pamoja ya kuleta mapinduzi chanya katika sekta ya elimu kupitia teknolojia.

“Kituo hiki kitakuwa kitovu cha ubunifu, mafunzo na majadiliano ya kitaaluma kati ya walimu wa Tanzania na wataalam kutoka China. Ushirikiano huu ni fursa ya kipekee kwa walimu wetu kupata ujuzi wa kisasa unaowandaa wanafunzi kwa dunia ya sasa na ya baadaye,” amesema Dkt. Mgonda.
Akizungumza kwa niaba ya Zhejiang Normal University, Huang Xiao ameeleza kuwa kituo hicho kinawakilisha mwanzo wa ushirikiano wa muda mrefu kati ya taasisi za elimu za China na Afrika.

“Walimu ndio msingi wa maendeleo ya jamii yoyote. Katika dunia ya sasa, ujuzi wa kidijitali si hiari tena bali ni hitaji. Kupitia mafunzo haya, tutashirikiana na walimu wa Tanzania si tu kwa maarifa, bali kwa kujenga uwezo endelevu wa kujifunza na kufundisha,” amesema Huang Xiao.
Ameongeza kuwa programu ya mafunzo itahusisha wataalam kutoka China katika nyanja za akili bandia, mbinu za kisasa za ufundishaji na elimu ya sayansi, huku akisisitiza kuwa ushirikiano huu unajenga daraja jipya la maendeleo ya elimu ya kidijitali kati ya China na Tanzania.
Uzinduzi wa Kituo cha Ushirikiano wa Elimu ya Kidijitali kati ya China na Afrika ni hatua muhimu katika kuleta mageuzi ya elimu nchini Tanzania. Kupitia ushirikiano huu, walimu wanapata fursa ya kujiimarisha kitaaluma, huku mfumo mzima wa elimu ukielekezwa kwenye matumizi ya teknolojia, ubunifu na ushirikiano wa kimataifa.