Na Lucy Ngowi
DODOMA: MWENYEKITI wa Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Dodoma, Ibrahim Sumbe amesema Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kushiriki makongamano ya ushirika ndani na nje ya nchi, ikiwa ni matokeo ya mshikamano na juhudi kubwa kutoka kwa vyama vya ushirika nchini.
Sumbe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya KKKT Arusha Road SACCOS, amesema hayo katika Maonesho ya Wakulima yajulikanayo kama Nanenane katika Viwanja vya Nzuguni Dodoma.

Amesema jukwaa hilo lilianzishwa miaka minne iliyopita kwa lengo la kuunganisha vyama vya ushirika wa kifedha (SACCOS) na vyama vya ushirika wa mazao (AMCOS), ili kushirikiana katika kutatua changamoto zinazowakabili kwa pamoja.
“Mafanikio yamekuwa makubwa. Kila chama hujifunza kutoka kwa kingine, na tumekuwa tukifanya shughuli mbalimbali kwa pamoja, zikiwemo za kijamii kama kutoa misaada kwenye vituo vya kulelea watoto yatima, watoto wenye ulemavu na wazee,” amesema.
Amesema Katika kipindi cha hivi karibuni, jukwaa hilo limetoa misaada yenye thamani ya zaidi ya Sh. Milioni 14 kwa Hospitali ya Mlowa, ambazo zimenunulia vitanda, mashuka na vifaa tiba mbalimbali.
Amesena kiwango cha mafanikio yao kimewafanya kutambuliwa kitaifa, ambapo jukwaa hilo lilishinda Tuzo ya Jukwaa Bora la Ushirika Kitaifa kwa mwaka huu.

Pia, wameshiriki katika maonyesho mbalimbali ya kitaifa na kimataifa, yakiwemo yale yaliyofanyika Uganda, Rwanda, na Kenya, wakionyesha bidhaa za kilimo na mazao mbalimbali.
“Inaonyesha jinsi Tanzania ilivyo mstari wa mbele karibu nusu ya wageni waliokuwepo kwenye makongamano haya walikuwa Watanzania. Tunaishukuru serikali kwa kutuunga mkono, ikiwemo hatua ya kuanzisha Benki ya Ushirika ambayo tayari imetengewa zaidi ya Sh. Bilionitano,” amesema.
Ametoa wito kwa Watanzania wote kujiunga na vyama vya ushirika akisisitiza kuwa, “Ushirika si chombo cha wanyonge kama ambavyo wengi wanavyodhani. Ni njia ya kuleta maendeleo ya pamoja, lakini mafanikio hayawezi kufikiwa bila umoja.”