Na Danson Kaijage
DODOMA: SERIKALI imepokea tuzo ya heshima katika mashindano ya Kimataifa ya Usalama wa Barabara kutokana na mchango wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
Mchango huo wa TANROADS ni katika kuboresha usalama wa barabara ili kupunguza hatari za ajali na kuhakikisha usalama wa watumiaji wote wa barabara, kupitia mpango wa Ten Step Plan Tanzania.

Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega ameiwakilisha serikali kupokea tuzo hiyo katika mkutano wa ‘Ten Steps to 2030 for Safer Road Infrastructure Side Event’ uliofanyika katika jiji la Marrakech nchini Morocco.
Taarifa iliyotolewa imesema kwamba mkutano huo ni wa nne wa Mawaziri kutoka Mataifa mbalimbali Duniani kuhusu Usalama Barabarani.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo TANROADS iimekuwa ni miongoni mwa washindani watano walioteuliwa kutoka nchi 11, baada ya kushindanishwa na taasisi nyingine 12 duniani.
Pia imesema mbali na TANROADS, taasisi nyingine zilizofikia hatua ya mwisho katika tuzo hiyo ni kutoka nchi za India, Australia, Peru na Saudi Arabia.
Taarifa imesema tuzo hiyo hutolewa kwa mamlaka na Wakala za barabara duniani zinazofanya juhudi kubwa za kuondoa barabara zenye hatari kwa watumiaji wake.
Waziri Ulega ameipongeza TANROADS kupitia Mtendaji mkuu wake Mohamed Besta kwa kazi nzuri inayoliletea taifa heshima na kuitangaza nchi duniani.