– Kiswahili Kuanza Kufundishwa Shuleni
Na Mwandishi Wetu,
COMORO: SERIKALI ya Tanzania na ile ya Muungano wa Visiwa vya Comoro zimekubaliana kuendeleza mashauriano yatakayowezesha kuanza kwa ufundishaji wa lugha ya Kiswahili katika shule za Comoro, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Saidi Yakubu ameeleza hayo akiwa pamoja na Waziri wa Elimu wa Comoro, Bacar Mvoulana, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kiswahili duniani yaliyofanyika katika mji wa Ntsaoueni, kisiwa cha Ngazidja.
Katika hotuba yake, Balozi Yakubu amesisitiza dhamira ya Rais Samia aliyoitoa mwaka jana wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya uhusiano kati ya Tanzania na Comoro, ambapo aliahidi kusaidia Comoro kwa kuipatia walimu pamoja na vifaa vya kufundishia Kiswahili.
Amesisitiza kuwa msaada huo utakuwa chachu ya kuimarisha matumizi ya Kiswahili visiwani humo, na kuongeza nafasi yake kama lugha ya mawasiliano ya kikanda.
Kwa upande wake, Waziri Mvoulana ameelezea shukrani za dhati kutoka kwa Serikali ya Comoro na kueleza kuwa tayari wizara yake imeanza maandalizi ya tathmini ya mahitaji muhimu kabla ya kuanza rasmi kwa mchakato wa ufundishaji wa lugha hiyo.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wakiwemo Gavana wa kisiwa hicho, mawaziri wa serikali ya Comoro, Balozi Mdogo wa Afrika Kusini, wawakilishi wa taasisi za kimataifa, mashirika ya kiraia, na wananchi kutoka miji 11 inayozungumza Kiswahili katika kisiwa cha Ngazidja.
Hatua hii ni mwendelezo wa juhudi za Tanzania kusambaza na kukuza lugha ya Kiswahili kimataifa, sambamba na kuimarisha diplomasia ya lugha kama chombo cha kuunganisha mataifa ya Afrika na kusukuma mbele maendeleo ya kijamii na kiutamaduni.