Na Mwandishi Wetu
MINSK: ZIARA ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa nchini Belarus imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili, baada ya kusainiwa kwa Hati Nne za Makubaliano katika sekta za mashauriano ya kisiasa, kilimo, elimu na biashara.
Makubaliano hayo yamesainiwa katika mji mkuu wa Belarus, Minsk, yalifikiwa baada ya mazungumzo rasmi baina ya Waziri Mkuu Majaliwa na mwenyeji wake Alexander Turchin, Waziri Mkuu wa Belarus.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mazungumzo hayo, Majaliwa amesema makubaliano hayo ni ishara ya utashi wa kisiasa uliopo baina ya Tanzania na Belarus katika kujenga ushirikiano wa kimkakati kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

“Hii ni ziara ya kwanza ya ngazi ya juu tangu tuanzishe uhusiano wa kidiplomasia mwaka 1996. Kusainiwa kwa hati hizi ni mwanzo wa ukurasa mpya wa ushirikiano unaolenga kuendeleza rasilimali zilizopo na kuleta maendeleo ya pamoja,” amesema.
Amesema kuwa kutokana na hatua kubwa za maendeleo zilizofikiwa na Belarus katika nyanja mbalimbali kama kilimo, elimu, Tehama, afya, nishati, viwanda na utalii, Tanzania imefungua milango kwa wawekezaji kutoka Belarus kuwekeza nchini.

Majaliwa ametaja maboresho ya sera na sheria za uwekezaji, miundombinu ya kisasa pamoja na motisha za kikodi kama sababu kuu zinazowavutia wawekezaji wa kimataifa.
“Tanzania ni lango la kibiashara Afrika. Tuna fursa ya soko la watu zaidi ya bilioni 1.6 kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), na Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA),” amesema.

Katika ziara hiyo, ujumbe wa Waziri Mkuu pia ulitembelea kiwanda cha kutengeneza dawa na vifaa tiba pamoja na kiwanda cha kutengeneza matrekta, ambapo walijionea teknolojia ya kisasa inayotumika katika uzalishaji.
Viongozi wa viwanda hivyo walieleza nia yao ya kushirikiana na Tanzania na wameahidi kufanya ziara ya kibiashara nchini hivi karibuni ili kuchunguza fursa zilizopo.
Ujumbe wa Waziri Mkuu uliambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Zanzibar, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi, pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Fredrick Kibuta.