Na Mwandishi Wetu, Mtwara
TANI 27,550 za ufuta zenye thamani ya sh bilioni 80 zimeuzwa na wakulima wa Mtwara, kupitia minada inayofanyika kwa kutumia mfumo wa Soko la Bidhaa Nchini (TMX).
Ofisa usimamizi wa Fedha kutoka TMX Prince Philimon amesema hayo wakati akizungumza na Mwandishi wa habari hii, kuhusu maendeleo ya minada ya ufuta ambayo inafanyika Mkoani hapa.
Philimon amesema tangu kuanza msimu wa uuzaji wa ufuta 2024/2025, minada sita imefanyika ambapo wakulima waliuza ufuta kwa bei ya juu ya shilingi 3,570 kwa kilo na bei ya chini ya shilingi 3,350.
Minada hiyo ambayo inaendeshwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi, Mtwara na Nanyumbu (TMX) ilizinduliwa June nne mwaka huu ambapo kwa mara ya kwanza walianza kutumia mfumo wa TMX.
Wakizungumza katika mnada wa sita ambao ulifanyika Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara, wakulima wa ufuta walieleza kufurahishwa na uuzaji wa ufuta kupitia mfumo huo wakisema unahamasisha upatikanaji wa bei nzuri Kwa kuleta wanunuzi wengi kwa wakati mmoja.
“Kwa kweli tunatamani mfumo huu utumike pia kwenye uuzaji wa mazao kama Korosho, mbaazi pia kwa sababu una manufaa sana hasa kwenye suala la bei, kama ulivyosikia bei inapanda kadri tunavyoendelea na minada, ” amesema Mkulima wa ufuta Nanyumbu Ally Omary.
Serikali ilitangaza utaratibu wa kununua zao la ufuta kupitia mfumo wa huo msimu 2024/2025 ili kuleta bei zenye ushindani, haki, uwazi, na kupunguza gharama za ununuzi wa zao hilo la ufuta Nchini.
Akizungumzia mienendo ya bei , Ofisa Usimamizi wa Fedha TMX Philimon amesema bei inapanda kadri minada unavyozidi kuendelea ambapo kwa sasa imefikia shilingi 3570 bei ya juu kwa kilo na 3350 ya chini.
Alisema mwanzo wa kutumia mfumo wa TMX wakulima walionyesha kutofurahishwa na mfumo lakin kadri minada ilivyozidi kufanyika kupitia mfumo huo na kuona manufaa yake wamekubali na kuomba utumike hata kwenye mazao mengine kama Korosho.