Na Danson Kaijage
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe amesema tafiti katika sekta ya afya ni nyenzo muhimu kuhakikisha huduma bora zenye tija kwa wananchi.
Dkt. Shekalaghe ametoa kauli hiyo jijini Dodoma, Aprili nne, 2025 wakati wa Ufunguzi wa Mdahalo wa Kitaaluma katika Maadhimisho ya Wiki ya Afya Kitaifa.
Amesema tafiti mbalimbali katika maeneo ya magonjwa yakiwemo malaria, kifua kikuu na yale ya kuambukiza, zimekuwa chachu ya mabadiliko chanya kwenye sera na mbinu za utoaji huduma.
Amesena serikali imeendelea kushirikiana na taasisi za utafiti, wadau wa maendeleo na sekta binafsi ili kuhakikisha tafiti zinazofanyika nchini zinagusa mahitaji halisi ya wananchi na kuchangia utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
“Tafiti zimetuwezesha kuwa na ushahidi wa kisayansi unaoongoza matumizi ya dawa mpya, mbinu bora za kinga na pia kubaini maeneo yenye changamoto kubwa zaidi kiafya,” amesema.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe amesema mdahalo huo wa kitaaluma utasaidia katika kusukuma mbele maendeleo ya sekta ya afya nchini.
Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Rashid Mfaume amesema hakuna halmashauri nchini isiyokuwa na hospitali, jambo linalothibitisha mafanikio ya uwekezaji mkubwa wa Serikali katika sekta ya afya.
Maadhimisho ya Wiki ya Afya kitaifa yenye Kauli mbiu isemayo, ‘Tulipotoka, Tulipo, Tunapoelekea; Tunajenga Taifa Imara Lenye Afya’ yanafayika kuanzia Machi tatu hadi nane, Aprili 2025
katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, jijini Dodoma,
Yanahusisha utoaji wa huduma za afya bure, maonesho ya taasisi, vipimo, chanjo pamoja na mijadala ya kitaalam.