Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: NAIBU Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel Maneno, ameipongeza Serikali kwa hatua kubwa ilizopiga katika kuimarisha mifumo ya kisheria nchini, hususan katika usimamizi na upekuzi wa mikataba ya Serikali, ambayo ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Akizungumza wakati wa maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea Dar es Salaam, Maneno amesema maboresho yanayofanywa na Serikali yanaonekana wazi kupitia shughuli zinazofanywa na taasisi mbalimbali, sekta binafsi na hata mtu mmoja mmoja, zinazoakisi mchango wao katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Amesema kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ina jukumu la kuishauri Serikali kuhusu masuala yote ya kisheria.
Katika kipindi cha mwaka 2024/2025, ofisi hiyo imeweka mkazo mkubwa katika kusimamia ubora wa mikataba ya umma, ambayo ina mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi.
“Serikali inaingia mikataba mingi ya ujenzi, huduma na uwekezaji, yote hii inahusisha fedha nyingi za umma zinazotokana na kodi za wananchi. Hivyo ni muhimu mikataba hiyo iwe bora, ifuatwe kwa mujibu wa makubaliano, na isilete migogoro itakayochelewesha utekelezaji wa malengo ya Serikali,” amesema.
Amesema ofisi yake inatoa ushauri wa kina kwa taasisi za umma kuhakikisha mikataba inayoingiwa inazingatia viwango bora vya kisheria, huku pia wakianzisha huduma za ushauri wa mapema ili kuzuia migogoro kabla haijatokea.
Maneno amesema mafanikio ya uzinduzi wa Juzuu za Sheria za Mwaka 2023, uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan Machi mwaka huu, 2025 Juzuu hizo zimefanyiwa urekebishaji kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2002 na sasa zinapatikana kwa urahisi kupitia tovuti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
“Kati ya sheria 446, takribani 300 zimetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili hii ni hatua muhimu ya kuhakikisha sheria zinaeleweka kwa wananchi wote, si kwa wanasheria pekee,” amesema.
Maneno amesema katika utekelezaji wa uwekezaji mkubwa nchini, ushauri wa kisheria hutolewa kabla ya kusaini mikataba, na majadiliano hayo hushirikisha sekta zote husika, kwa kuzingatia sheria za ndani na zile za kimataifa.
“Taasisi zote husika zinahusishwa katika hatua mbalimbali za majadiliano. Kazi yetu kubwa ni kuhakikisha mikataba hiyo inaleta manufaa kwa nchi, inalindwa kisheria, na utekelezaji wake una tija kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema.