Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: NAIBU Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, upande wa taaluma Profesa Bonaventure Rutinwa ametoa wito kwa Taasisi ya Kichina ya Confucius kuhakikisha kwamba vitabu vinavyozinduliwa na vitakavyoandikwa baadaye vinakuwa na rasimu ya Kiswahili.
Profesa Rutinwa ametoa wito huo wakati wa uzinduzi wa Kitabu cha kujifunza lugha ya kichina kilichotafsiriwa kwa lugha ya kiswahili chuoni hapo ili kuwawezesha wanafunzi wa kitanzania wanaojifunza lugha hiyo kuelewa kwa haraka.
Amesema, “Nimeelezwa kwamba Mheshimiwa Palamagamba Kabudi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amewahi kutoa ushauri kwa Taasisi ya Confucius kutafsiri hotuba za Mheshimiwa Xi Jinping kwa Kiswahili.
“Ninakuhimizeni kuupa uzito ushauri huo na kuzingatia kuwa ushauri wa Mheshimiwa Waziri ni maelekezo,”.
Amesema imani yake ni kwamba, wachapishaji kampuni ya Changjiang Publishing & Media Co. Ltd kutoka China, watakuwa tayari kuchapisha vitabu hivyo kama mchango wao katika kuimarisha uhusiano baina ya China na Tanzania.
Amesema kitendo hicho ni chachu ya kukuza ujuzi wa lugha ya Kichina miongoni mwa wanafunzi wa Tanzania.
“Uandishi wa kitabu hiki ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya chuo yanayohusu utafiti na uchapishaji. Hongereni sana Taasisi ya Confucius kwa kazi hii ya kutiliwa mfano,” amesema.
Amesema kitabu hicho kipya kilichoandikwa na wakurugenzi na walimu wa Taasisi ya Confucius kimepokelewa kwa matumaini makubwa kuwa kitaongeza uelewa wa Watanzania kuhusu sera za China na kuchochea tafakuri pana kuhusu ushirikiano wa nchi hizo mbili.
Mkurugenzi wa Taasisi hiyo upande wa China hapa Tanzania, Profesa Zhang Xiaozhen,, amesema Rais wa China, Xi Jinping , amekuwa akisisitiza umuhimu wa kujengwa ushirikiano wa kiutamaduni na hatimaye kuifanya jamii kuishi kwa ushirikino na kuifanya dunia kuwa sehemu salama na rafiki.
“Hivyo kupitia kitabu hiki ni mwendelezo wa kutimiza maono hayo ya Rais wetu ambapo wajifunzaji wa lugha ya kichina sio tu kitawafanya kujifunza lugha ya kichina bali kupata taarifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na shughuli za kiutamaduni kuhusu nchi ya China.
Amesema kitabu hicho kinaitwa “Mtazamo wa jumla kuhusu China’ kitawanufaisha wanafunzi watakaojifunza lugha ya kichina wakiwemo wanaosomea stahahada na shahada ya lugha ya kichina na wale wanaosomea ngazi ya cheti na kozi fupi katika lugha hiyo.
Profesa Zhang amesema katika uandishi wa kitabu hicho, mambo yaliyozingatiwa ni pamoja na ukweli ili kuhakikisha mwanafunzi anakuwa na uelewa mzuri katika ujifunzaji wake na kuepuka kukutana na changamoto zisizo za lazima.
“Taarifa zilizopo ndani ya kitabu hicho zimetoka katika vyanzo vya kuaminika na pia vimewekwa mazoezi mbalimbali vitavyowasaidia wasomaji wake,”amesema Mkurugenzi huyo.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Kichina upande wa Tanzania, Dkt. Hans Mussa, amesema kitabu hicho kitawanufaisha wanafunzi watakaojifunza lugha ya kichina wakiwemo wanaosomea stahahada na shahada ya lugha ya kichina, wanaosomea ngazi ya cheti na kozi fupi.
Dkt. Musa amesema kitabu hicho kina sura 12 na mada 19 zinazolenga maeneo mbalimbali ikiwemo kuhusu China , lugha na maandishi ya kichina, Miji mikuu ya Kale ya China, miji maarufu nchini China.