Na Mwandishi Wetu
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Tulia Ackson ametaka kujua kuhusu mwongozo wa watu wanaojitolea kazini kama umetoka akielekeza swali hilo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene.
Amefafanua hayo Bungeni na kuongeza kuwa kama mwongozo huo haujatoka liwekwe bayana na kama linahitaji mawazo mapana basi wanaweza kushirikishwa watu wengi zaidi.
“Mngetusaidia hili kwa sababu ajira zimetolewa hivi karibuni na nitaenda kwenye mfano mmoja wapo, kuna madaktari ambao wako hospitalini kwa mkataba huo huo wa kujitolea kwa sababu wanalipwa nusu hawa wanawafunisha wale wanaokuja kama ‘Intern’ halafu wanaajiriwa intern nao wanaachwa wakati wote waliomba”, amesema Dk Tulia.
Amehoji ni vigezo gani vya kupokea intern (wale wanaopewa mafunzo kazini) wakati aliyempokea na kumfundisha kazi anaachwa, hivyo suala hilo litazamwe kwani yanawaumiza watoa huduma.
“Nimetoa mfano wa madaktari kwani kwenye jimbo langu ziko nyingi lakin ni hoja hio hio kwa kada nyingine kama walimu, manesi na wengine pia,” amesema.
Hoja ya Spika imetokana na wabunge kuuliza kuhusu walimu waliojitolea kwa muda mrefu iwapo wamezingatiwa kwenye ajira mpya zilizotangazwa.
Katika majibu yake Simbachawene amesema kuwa mwongozo huo utatolewa japokuwa kuna changamoto kwenye vigezo lakini wanashirikiana na kamati walijadili kwa pamoja kwa sababu vigezo vinasumbua sana.