Mwandishi Wetu
KIGOMA: MKUU wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amezihimiza halmashauri zote katika Wilaya ya Kasulu kuhakikisha zinatenga maeneo rasmi kwa ajili ya uwekezaji, hatua itakayowawezesha wawekezaji kupata ardhi kwa urahisi bila vikwazo vya kisheria au kiutendaji.
Akizungumza katika mkutano wa kujitambulisha kwa viongozi wa Serikali, watumishi wa umma, viongozi wa dini, wazee maarufu na wananchi, uliofanyika kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Sirro amesema uwekezaji ndio njia muhimu ya kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika mkoa huo.

“Nafahamu wilaya yetu ina fursa nyingi kupitia kilimo cha mazao ya chakula na biashara, pamoja na utalii. Nisisitize tu watendaji kuongeza ubunifu, kuweka mifumo mizuri ya usimamizi, na kushirikiana kwa karibu na wawekezaji wote ili kuongeza pato la wilaya, mkoa na taifa,” amesema.
Kwa kuzingatia jiografia ya mkoa wa Kigoma unaopakana na mataifa yenye changamoto za kiusalama, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka watumishi wa umma kutoa elimu ya uraia kwa wananchi, ili kuhakikisha wageni wanaoingia nchini wanaheshimu sheria, kanuni na taratibu zilizopo, kwa lengo la kulinda amani na mshikamano.

Sirro amesisitiza umuhimu wa kuzingatia vipaumbele vya mkoa, hasa katika usimamizi wa miradi ya maendeleo, utekelezaji wa sera ya matumizi bora ya ardhi, kukuza biashara na uwekezaji, pamoja na kuboresha huduma za jamii kama elimu, afya na upatikanaji wa maji safi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Isaac Mwakisu amesema hali ya usalama katika wilaya hiyo ni ya kuridhisha, huku akisisitiza kuwa maeneo yaliyotengwa kwa wawekezaji tayari yatalindwa kwa gharama yoyote ili kuendeleza mazingira bora ya biashara.

Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini, Joyce Ndalichako ameungana na viongozi hao kwa kusisitiza kuwa utekelezaji wa Ilani ya Chama Tawala umeleta mafanikio makubwa wilayani humo, huku akitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutimiza dira ya maendeleo.