Na Danson Kaijage
DODOMA: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema serikali imefanikiwa katika mpango wa Miradi ya kutoa ajira za muda katika kunusuru Kaya Maskini nchini.
Simbachawene amesema hayo wakati akitoa taarifa ya mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa upande wa Mfuko wa maendeleo ya Jamii (TASAF). katika ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO Jijini Dodoma.

Amesema hadi kufikia Disemba, 2024, jumla ya miradi 27,863 ya kutoa ajira za muda kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini imetekelezwa.
Amesema katika miradi hiyo Kaya za walengwa 662,000 zimelipwa Sh. Bilioni 213.8.
Pia amesema licha ya kuongeza kipato, walengwa pia wameweza kupata ujuzi wa utekelezaji wa miradi hiyo unaoweza kutumika katika shughuli za kukuza uchumi wa kaya na kuongeza kipato katika sekta za kilimo, barabara, misitu, maji na mazingira.

Ameelezea mafanikio mengine ni pamoja na miradi ya kuendeleza na kuboresha Miundombinu ya huduma za Jamii Jumla ya miradi 137 ya uendelezaji miundombinu yenye thamani ya Sh Bilioni 12.67 ilitekelezwa katika mamlaka za maeneo ya utekelezaji 29.
Amesema kati ya miradi hiyo miradi sita imekamilika na 72 ilikuwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
“Miradi ya aina hii imetatua changamoto za jamii zinazotokana na upungufu au kutokuwepo kabisa kwa miundombinu ya kutosha ya kutolea huduma za jamii katika sekta za elimu, afya na maji.
“Miradi ya Kupunguza Umaskini Tanzania-Awamu ya Nne
hadi kufikia Disemba, 2024, jumla ya miradi ya jamii 1,518 yenye thamani ya Sh. Bilioni 81.8 imetekelezwa ambapo miradi 659 imekamilika na inatumika kutoa huduma na miradi 859 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
” Idadi ya miradi hiyo kisekta ni elimu 495, afya 262, barabara za Vijijini 120, maji 23,kilimo 11, mazingira sita, majosho manne na miradi ya kuongeza kipato 597,” amesema.
Amesema miradi ya kuondoa umaskini awamu ya nne, unatekelezwa na TASAF kwa ufadhili wa Umoja wa Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa wingi Duniani (OPEC) katika mikoa mitano ya Arusha, Geita, Mwanza, Njombe na Simiyu.
Ametaja mafanikio mengine ya TASAF kuwa ni pamoja na mpango wa kutoa mafunzo ya Stadi za Msingi za kiuchumi na ruzuku ya uzalishaji kwa walengwa.
Pia amesema hadi kufikia Disemba, 2024, walengwa 94,520 kwenye mamlaka na maeneo ya utekelezaji 69 walikuwa wamepewa ruzuku ya uzalishaji ya Sh. Bilioni 35.9 kama mtaji kwa ajili ya utekelezaji wa miradi waliyokuwa wamebuni.
Vile vile TASAF inahamasisha kaya zenye watoto walio katika umri wa kwenda shule kuhakikisha watoto wao wanahudhuria masomo kwa asilimia zaidi ya asilimia 80 ya siku za masomo kwa mwezi.
Amesema TASAF kwa kushirikiana na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imewezesha waombaji wa mikopo ya elimu ya juu kutoka kaya za walengwa kutambulika, kupatiwa mikopo ya elimu kwa asilimia 100.
Hadi kufikia Novemba 2024 jumla ya wanafunzi 8,274 wamenufaika na mikopo hiyo.
Ameeleza kwamba kumekuwepo na kuboreka kwa hali ya walengwa
Katika Utekelezaji wa afua mbalimbali, TASAF imefanikiwa kuhitimisha kaya za walengwa takribani 400,000 nchi nzima.