Na Danson Kaijage
DODOMA: SHEIKH wa Mkoa wa Dodoma, Alhaji Mustapha Rajabu, amekemea vikali vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kuelekea uchaguzi mkuu.
Rajab amewataka wananchi kutokubali kupokea rushwa na wasiwachague wagombea wanaojihusisha na vitendo hivyo.

Akizungumza muda mfupi baada ya Swala ya Ijumaa, Sheikh Rajab amesema tayari kumekuwepo na viashiria vya wagombea kutoa rushwa wakati wa mchakato wa kura za maoni, jambo ambalo linahatarisha maadili ya uongozi na ustawi wa taifa.
“Rushwa ni adui wa haki. Kiongozi anayetoa au kupokea rushwa ni mtu mdhulumu, asiyestahili kuaminiwa na wananchi,” amesema.
Kutokana na ongezeko la vitendo vya rushwa, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Dodoma, kwa kushirikiana na Ubalozi wa Saudi Arabia kupitia Idara ya Dini ya Kiislamu, wameanzisha semina na makongamano maalumu ya kutoa elimu kuhusu madhara ya rushwa na umuhimu wa kuikataa.
Sheikh Mustapha aliwataka viongozi wa dini, wazazi, na walezi kushirikiana katika kuwaelimisha wananchi ili waweze kufanya maamuzi sahihi bila kushawishiwa kwa rushwa.