Na Lucy Ngowi
DODOMA: MBUNGE wa Kilombelo, Abubakary Asenga ameiuliza Serikali ni utaratibu gani unaopaswa kufuatwa na wananchi wanaofanya biashara pembezoni mwa barabara zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS,) hususan katika maeneo ya Mkambe, Kidatu na Mkula.
Katika swali la nyongeza, Mbunge huyo ametaka kujua ni lini wananchi ambao hawajalipwa fidia kupisha ujenzi wa barabara ya Ifakara–Kidatu watalipwa stahiki zao.
Aidha, amehoji ni lini taa za barabarani katika barabara hiyo zitafungwa.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, amesema kuwa kwa mujibu wa Marekebisho ya Kanuni za Matumizi ya Barabara za Mwaka 2025, Kanuni ya 36(4) imeweka utaratibu mahsusi kwa wafanyabiashara wanaotaka kutumia maeneo yaliyopo pembezoni mwa barabara.
Amefafanua kuwa mfanyabiashara anatakiwa kujaza fomu maalum ya maombi inayotolewa na TANROADS na kulipia ada ya maombi kabla ya kuwasilisha fomu hiyo.
Amesema baada ya kupokea maombi, TANROADS itayachakata na yale yatakayokidhi vigezo yatapatiwa kibali pamoja na kuarifiwa gharama zinazopaswa kulipwa kwa mujibu wa sheria.
Kuhusu fidia, Kasekenya amesema kuwa Kamati imeundwa chini ya Mkuu wa Wilaya kwa ajili ya kusikiliza malalamiko ya wananchi ambao hawajalipwa au wamepata upungufu wa fidia, baada ya Serikali kujiridhisha kuwa wanastahili, wananchi hao watalipwa fidia zao.
Kuhusu taa za barabarani, alisema kuwa kuna taratibu zinazoendelea za uwekaji wa taa, na kwamba barabara zote mpya, ikiwemo Ifakara–Kidatu, zitawekewa taa za barabarani.

