Na Lucy Ngowi
SERIKALI imetoa zabuni kwa kampuni ya kizalendo kwa ajili ya kufanya utafiti katika Bahari ya Hindi ili kujua ni aina gani ya meli ya mizigo inapaswa kuwepo kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya nchi.
Utafiti huo utahusu ukubwa wa meli inayopaswa kuwepo kutokana na soko lilivyo, ambayo itakuwa na uwezo wa kufanya kazi kwenye mwambao, Bahari ya Hindi ama nje ya nchi.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli nchini, Eric Hamissi amesema hayo alipozungumza na Mwandishi Gazeti la Mfanyakazi.
Amesema meli hiyo itafanya kazi ya kubeba mizigo lakini pia wanafunzi wanaosoma Chuo cha Bahari watafanya mazoezi ya vitendo kupitia meli hiyo.
Wakati Mkurugenzi huyo akielezea hayo katika siku za karibuni Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Mabaharia Tanzania (TASU), Hamis Urembo aliiomba serikali inunue meli au kutengeneza kwa ajili ya kupeleka mizigo nje ya nchi na kuileta Tanzania ili vijana wanaomaliza chuo wapate ajira.
Urembo alitoa ombi hilo kwa kuwa hivi sasa ajira za mabaharia zimekuwa chache, ilhali chuo cha baharia kikiwa kinazalisha wanafunzi wengi kila mwaka ambao wanazagaa mitaani kwa kuwa hakuna meli ya kuwasaidia.
Kwa maelezo ya Urembo, zamani kulikuwa na kampuni ya ushirikiano ya meli ya China na Tanzania, kulikuwa na meli nyingi, hivyo kupitia chama cha mabaharia kila baada ya miezi sita, mabaharia wa Tanzania walienda China, walifanya kazi kwa kupokezana na wengine kwa mkataba wa miezi sita.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Huduma za meli nchini Hamissi amesema, utafiti huo utakapokamilika, mwaka ujao wa fedha 2025/ 2026 watakuwa wamejua aina gani ya meli wanaanza kuijenga au kuinunua.
Kwa upande mwingine Hamissi amesema serikali inajenga kiwanda kikubwa cha kujenga meli Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma.
Amesema meli ya uzito wa tani 5000 ndio itakayojengwa katika kiwanda hicho.
“Mpaka sasa tumeshasaini mikataba na wakandarasi hivyo muda wowote ujenzi wa kiwanda hicho utaanza,” amesema.
Kiwanda hicho kinagharimu sh bilioni 322.
Akiwa katika Jukwaa lililoandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile alisema katika kuboresha sekta ya uchukuzi serikali ina mpango wa kujenga meli mpya mbili za kisasa, jambo litakaloleta mageuzi makubwa nchini.
Pia alisema serikali inajenga kiwanda kipya cha kutengeneza na kukarabati meli ambacho hakijawahi kujengwa katika bara la Afrika.