Na Mwandishi Wetu
NCHI wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimetakiwa kudumisha mshikamano na utekelezaji thabiti wa malengo yao ili kufanikisha ukombozi wa kiuchumi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Zimbabwe, Profesa Amon Murwira, ametoa wito huo jijini Antananarivo, Madagascar, alipokuwa akikabidhi uenyekiti wa Baraza la Mawaziri kwa mwenzake wa Madagascar, Rasata Rafaravavitafika, Tanzania iliwakilishwa na Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
Profesa Murwira alikumbusha kuwa mafanikio ya jumuiya hiyo yanahitaji dhamira ya kweli na kushinda changamoto zilizopo.

Amewakumbusha washiriki kuhusu maono ya waanzilishi wa SADC kama Mwalimu Julius Nyerere na Robert Mugabe, akisisitiza umuhimu wa mshikamano wa kikanda.
Katibu Mtendaji wa SADC, Elias Magosi, ameeleza kuwa mkutano huo umejikita katika tathmini ya utekelezaji wa dira ya maendeleo, hususan kwenye viwanda, biashara na ushirikiano.
Ametaja changamoto za sasa kama vile mabadiliko ya kisiasa kimataifa, ongezeko la kodi, na kupungua kwa misaada ya wahisani, akihimiza nchi kujitegemea zaidi.
Aidha, ameeleza kuwa SADC inaendelea kuimarisha sekta ya biashara ndogo na za kati, ambazo zinachangia ajira kwa vijana na wanawake, ingawa zinakumbwa na changamoto za ujuzi, mitaji na masoko.

Ili kukabiliana nazo, jumuiya hiyo imeandaa mkakati wa kuongeza ushindani ndani ya soko la Afrika (AfCFTA).