Na Mwandishi Wetu
BALOZI wa Tanzania Jamhuri ya Czech mwenye makazi yake Berlin, Ujerumani, Hassani Iddi Mwamweta, amesaini mkataba wa kuhuisha nafasi ya Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Czech, Roman Glorig.

Glorig ambaye ni mmiliki wa kiwanda cha kutengeneza ndege cha Airplane Africa Limited kilichopo mkoani Morogoro, ataendelea kuiwakilisha Tanzania kwa heshima katika Jamhuri ya Czech, hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Mkataba huo ulisainiwa kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, ni ishara ya kuendeleza na kupanua uhusiano wa kidiplomasia uliopo.

Tukio hilo linaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Tanzania ya kukuza mahusiano ya kimataifa, hususan katika maeneo ya afya, elimu, biashara, uwekezaji na utalii.
Kupitia ushirikiano huu, Serikali inatarajia kuongeza ubadilishanaji wa ujuzi kati ya wananchi wa Tanzania na Czech, kuimarisha mikakati ya kutangaza bidhaa na vivutio vya utalii vya Tanzania, pamoja na kuvutia wawekezaji wapya kutoka Czech.
Aidha, hatua hii inatarajiwa kuunga mkono juhudi mbalimbali za kijamii zinazolenga kuinua maisha ya wananchi na kuchangia maendeleo endelevu ya Taifa.

Kwa kuendeleza uwakilishi wa heshima kama huu, Tanzania inaendelea kudhihirisha msimamo wake wa kujenga mahusiano ya kimkakati na washirika wa maendeleo duniani, kwa manufaa ya taifa na watu wake.