Na Mwandishi Wetu
PWANI: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete amepokea msaada wa vifaa tiba kwa ajili ya Hospitali ya Msoga na madawati 120 kwa ajili ya Shule za Msingi mbili za Chalize mkoani Pwani.
Ridhiwani Kikwete ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze ameshukuru kwa msaada huo uliotolewa na Benki ya NMB Chalinze na kushauri sekta binafsi kushirikiana na serikali kutatua changamoto mbalimbali za wananchi.
“Kwa mujibu wa takwimu za makusanyo na mapato, NMB- Chalinze ndiyo tawi namba moja Tanzania kwa hiyo maana yake NMB wanapozungumza tunapata Bilioni 500 ni pamoja na mchango mkubwa wa Chalinze,” amesema.
Amesema kwa ushirikiano wa serikali na sekta binafsi kutakuwa na uchumi endelevu, pia sekta hizo binafsi zinarudisha kwa wananchi kile wanachokipata.
Amesema Katika tukio hilo wengine walioshuhudia ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, Mkurugenzi wa Halmashauri Ramadhani Possi na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze Hassani Mwinyikondo.
Katika utoaji wa msaada huo NMB iliongozwa na Mkuu wa Idara ya Mitandao ya Matawi na Mauzo, Renatus Richard.