Na Lucy Ngowi
MOROGORO: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete ameiagiza Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), kushughulikia migogoro kwa haraka, ufanisi na weledi ili kutimiza matarajio ya wadaawa na wadau ambao wengi wao ni wawekezaji, kusaidia kukuza Uchumi wa nchi.
Ridhiwani ameagiza hayo alipofungua akifungua kikao kazi cha Tathmini ya Utendaji Kazi na mafunzo kwa watumishi wa CMA, Mkoani Morogoro.
Amesema kwa kufanya hivyo kutachochea ukuaji wa kiuchumi na kuhakikisha mahala pa kazi panakuwa na amani ili kuwafanya wafanyakazi na waajiri watumie muda mwingi kufanya uzalishaji wenye tija.

Ridhiwani pia ameitaka tume hiyo kuwa taasisi ya kimkakati katika utatuzi wa migogoro ya kikazi.
“Serikali iliongeza bajeti ya tume kiasi cha zaidi ya Sh. Milioni 900,000 bila shaka mmeona ongezeko hilo limeleta mabadiliko siyo tu kwenye maslahi ya wafanyakazi lakini pia kuiwezesha tume kutekeleza majukumu yake ya msingi,” amesema.
Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Dkt. Yose Mlyambina amewakumbusha wasuluhishi na waamuzi kutilia mkazo suala la matumizi ya mfumo wa kielekroniki, kuangalia namna bora ya kupokea vielelezo ili kuwasilisha jalada kamilifu pindi litakapoitishwa mahakamani.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa CMA, Usekelege Mpulla ameeleza kuwa tume hiyo itaendelea kuwa taasisi ya kimkakati katika kukuza uchumi nchini kwa kuimarisha utatuzi wa migogoro ya kikazii ili kuhakikisha mahala pa kazi panakuwa na amani.
Amesema kwa kufanya hivyo wafanyakazi na waajiri watatumia muda mwingi kufanya uzalishaji wenye tija.