Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete ameitaka bodi ya Ushauri wa Masuala ya Kazi, Uchumi na Kijamii (LESCO), kuendelea kushirikiana na serikali ili sekta ya kazi na ajira izingatie misingi ya kazi zenye staha.
Ridhiwani ameeleza hayo alipokutana na bodi hiyo ofisini kwake ambayo inakaribia kumaliza muda wake wa miaka mitatu ya kazi.

“Pamoja na kuwapongeza ninawaomba muendelee kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuhakikisha sekta ya kazi na ajira inazingatia misingi ya kazi zenye staha kwa maslahi ya wafanyakazi na waajiri,” amesema.
Mwenyekiti wa LESCO Dkt. Samwel Nyantahe ameishukuru serikali kwa kutoa ushirikiano katika kipindi cha utekelezaji wa majukumu yao.
Uongozi wa Baraza hilo unamaliza muda wake Septemba 12, 2024 na kwa sasa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imeanza mchakato wa kuwapata wajumbe wengine.