Na Lucy Lyatuu
WAZIRI Wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira Vijana Na Wenye Ulemavu ,Ridhiwan Kikwete amezindua jengo la kimkakati la biashara linalomilikiwa na Shirikisho La Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) lililoko jijini Arusha.
Jengo hilo lenye vyumba vya biashara, ukumbi wa mkutano, hoteli na maeneo mbalimbali yanayotumika kibiashara limejengwa na kukarabatiwa na kampuni tanzu ya TUCTA inayojulikana kama WDC.
Akizungumza,Kikwete amesema
Ufunguzi wa jengo hilo la kisasa ni ishara ya wazi kuwa wafanyakazi nchini wameamua kwa dhati kuunga mkono maendeleo na kuimarisha ustawi wa jamii yetu kiuchumi.

Wahenga walisema: “Kidole kimoja hakivunji chawa.” Hii ni kusema kuwa mshikamano ni nguzo ya maendeleo ya kweli. Vyama vya wafanyakazi vikiwa imara, taifa linakuwa imara. Vinatoa mchango mkubwa katika kudumisha amani, utulivu na maendeleo ya taifa” amesema.
Amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango huo, hasa katika kulinda haki za wafanyakazi, kukuza ustawi wao, na kuhimiza uzalishaji pamoja na utoaji wa huduma zenye tija kwa taifa letu.
“Hakuna anayeshinda kivyake — tunashinda pamoja, na kufurahia ushindi pamoja!Maana ya Jengo hili kwa Mustakabali wa TUCTA,” amesema.

Amesema Ujenzi wa jengo hilo ni ushahidi kwamba ndoto huweza kutimia kupitia mshikamano.
“Jengo hili si kuta na dari pekee — bali ni chimbuko la fikra mpya, mikakati madhubuti, na sauti ya wafanyakazi,” amesema.
Aidha amesema amefarijika kusikia kwamba katika jengo hilo kuna Wapangaji ambao ni Wafanyabiashara Wakubwa na Wadogo 115 ambao huwezesha kupata mapato ya Sh Milioni 50 kwa mwezi.
Amesema Kwa uwekezaji huo mzuri wa Kimkakati, ni vema TUCTA ikaona uwezekano wa kuongeza vitega Uchumi kwenye maeneo mengine Nchini.
Kikwete ametoa rai kwa TUCTA na vyama vyake vyote kulitumia jengo hilo kama kituo cha mafunzo, mazungumzo ya kijamii, na kuleta mabadiliko chanya katika mazingira ya kazi.
Amewakumbusha kuwa , migogoro na migongano ni sumu kwa mshikamano na ni kikwazo kwa ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii.
Amesisitiza kwamba, jengo linaweza kujengwa kwa saruji na chuma, lakini mshikamano hujengwa kwa uaminifu, uadilifu, uzalendo, mazungumzo ya kweli na nia njema.
“”Dumisheni mshikamano miongoni mwa Vyama vya Wafanyakazi, Dumisheni mshikamano na Waajiri, bila kuwasahau Wafanyakazi ambao hutoa mchango mkubwa wa Nguvukazi katika uzalishaji,
Naomba jengo hili liwe taa ya mshikamano wa wafanyakazi nchini na liwe kielelezo cha mafanikio ya umoja wenu,” amesema.

Amewataka kutimiza wajibu kwa mujibu wa Katiba ya Nchi, Sheria zilizopo na Katiba za vyama vya wafanyakazi.
“Wajibikeni kwa kila eneo mnalohusika nalo na muendelee kutoa michango chanya kwa maendeleo na ustawi wa taifa letu,” amesema.