Kongamano La STICE Dar
Na Lucy Ngowi
DODOMA: RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua rasmi mfuko wa mikopo wenye kianzio cha Sh. bilioni 2.3 kwa ajili ya kusaidia ubidhaishaji na ubiasharishaji wa bunifu na teknolojia zinazobuniwa na vijana wa Kitanzania.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema hayo Katika Mkutano na Waandishi wa Habari uliohusu Kongamano la Tisa la Kitaifa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (STICE), litakalofanyika Dar es Salaam.
Profesa Mkenda amesema Rais Samia pia atakabidhi hundi yenye thamani ya Sh. bilioni 6.3 kwa watafiti 19 katika masuala ya mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo nishati safi ya kupikia.
“Pia Samia atawatambua na kutoa tuzo maalumu kwa wanasayansi na wabunifu ambao matokeo ya kazi zao yamechangia kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii, ndani na nje ya nchi,”amesema.
Amesema kabla ya hafla ya ufunguzi wa kongamano hilo, Rais Samia atapata fursa ya kutembelea maonesho ili kujionea baadhi ya matokeo ya utafiti na ubunifu ambayo yamechangia katika kubadili mfumo wa kiuchumi na kijamii hapa nchini.
“Hii ni fursa adhimu kwa watafiti na wabunifu nchini kuthibitisha mchango wa sayansi, teknolojia na ubunifu katika maendeleo ya nchi yetu, hivyo ninawaasa washiriki kwa wingi katika maonesho hayo,”amesema.
Amewaalika watanzania na wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi, ndani na nje ya nchi, kushiriki Kongamano hili la STICE kwani ushiriki wao ni muhimu katika kuleta mawazo na mikakati mipya, kuimarisha utafiti na ubunifu, na kuhakikisha kuwa matokeo ya utafiti na ubunifu yanajibu mahitaji na kutatua changamoto za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
88
Kongamano hilo linalofanyika kila mwaka chini ya uratibu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) lenye lengo la kuwaleta pamoja watafiti, wabunifu, na wadau kutoka sekta mbalimbali, ndani na nje ya nchi, ili kujadili, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha mchango wa sayansi, teknolojia na ubunifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.