Na Mwandishi wetu
MOROGORO: WAGENI zaidi ya 800 kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) wamefanya ziara ya kihistoria katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro.
Ziara hiyo ambayo imefanyika baada ya wajumbe wa TUGHE kumaliza semina iliyofanyika jijini Arusha, lengo lake ni kuwaweka pamoja waajiri na wafanyakazi ili kupata uelewa wa pamoja, kujadili na kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza mahala pa kazi.
Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Joel Kaminyoge amesema lengo la ziara yao ni kutoa hamasa ya utalii wa ndani na kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza utalii ambapo ziara hiyo imewapa fursa wanachama wao kujionea vivutio vya kipekee vinavyopatikana hifadhi ya Ngorongoro.

“Leo tumekuja na wanachama zaidi ya 800 kutembelea Kreta ya Ngorongoro kujionea moja kati ya vivutio bora vya dunia ambavyo ni sehemu ya urithi wa dunia,
“Tunaamini kwamba ziara yetu italeta tija na hamasa kwa wakuu wa taasisi kuwa na utaratibu wa kuwapeleka watumishi wao kufanya utalii wa ndani katika vivutio mbalimbali nchini,” amesema.
Naye Meneja wa huduma za Utalii na masoko wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Mariam Kobelo amesema mamlaka hiyo ipo tayari kuendelea kupokea makundi mbalimbali ya wageni na kuwahakikishia kuwa wanapata huduma bora ili kuendelea kutangaza hifadhi hiyo na kuimarisha utalii ndani.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tanzanite Cooperates L.t.d aliyeratibu ziara hiyo, Elina Mwangomo, ameleza kuwa kwa sasa kuna ongezeko kubwa la watalii wa ndani hali inayoongeza hamasa kwa wadau wa utalii kuendelea kuboresha huduma zao.
Amesema Ngorongoro imekuwa moja kati ya eneo ambalo linapendwa zaidi na wageni na watalii kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Kwa upande wake, Jackline Ngoda ambaye ni mmoja kati ya wanachama waliotembelea Hifadhi hiyo ameonesha kufurahishwa na ziara hiyo baada ya kujionea wanyama mbalimbali ikiwepo wanyama wakubwa watano wakiwa katika maeneo yao ya asili.
“Kwa ujumla tumeona Wanyama mbalimbali, wakiwemo Simba, Nyati, Tembo, Swala, nyumbu, viboko, pundamilia na wengine wengi, tumeweza kuona uzuri wa kipekee wa Kreta ya Ngorongoro na napenda kuwaambia watanzania wenzangu waje kutembelea Ngorongoro na kujionea uzuri wake wa asili,” amesema.