Na Lucy Ngowi
DODOMA: RAIS Samia Suluhu Hassan, amemtaka Waziri Mkuu mpya wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, kuepuka vishawishi kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki, badala yake ajikite zaidi katika kuwatumikia Watanzania.
Samia ameyasema hayo, leo Novemba 14, 2025 muda mfupi baada ya kumuapisha Nchemba katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma.

Amemtaka Mwigulu kusimamia kikamilifu utekelezaji wa ahadi walizowapa wananchi wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu.
“Kwa umri wako, mzigo huu ni mkubwa na vishawishi ni vingi kutoka kwa marafiki, ndugu, jamaa na wengine. Nafasi yako hii haina rafiki, haina ndugu, haina jamaa ni nafasi ya kulitumikia Taifa. Nakutakia kila la kheri katika utumishi wako,” amesema.
Rais Samia amesisitiza umuhimu wa kutumia muda uliopo kutekeleza ahadi za Serikali kwa wananchi.
Pia amemtaka kutumia uzoefu wake katika Wizara ya Fedha kusimamia vyema baraza la Mawaziri, pamoja na kuhakikisha kuwa Waziri wa Fedha anatimiza wajibu wake ili upatikane ufadhili wa kutekeleza miradi ya maendeleo.


