Na Lucy Lyatuu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi ambaye ndiye mgeni rasmi katika ufunguzi katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam 2025, ‘Saba Saba’ anatarajiwa kukata keki kubwa ambayo ina kilogramu 3000 sawa na tani tatu.
Aidha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Palamagamba Kabudi amefurahishwa na keki kubwa ambayo imetengenezwa na kubuniwa miradi mikubwa iliyotekelezwa na serikali ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake.
Waziri Profesa Kabudi ameeleza furaha yake baada ya kutembelea banda la kampuni ya kutengeneza keki na mikate ya Lazziz Bakery Limited katika maonesho huku akibainisha kuwa kilichomvutia ni kuonesha mambo makubwa yaliyopatikana katika serikali ya Dk. Samia Suluhu Hassan.

Amefafanua kuwa miradi ambayo imetekelezwa katika serikali ya Dk.Samia ni pamoja na kupunguza vifo vya uzazi kwa asilimia 80.
Profesa Kabudi ameeleza kuwa Keki hiyo inawasilisha aina ya ubunifu kwa kuonesha mambo yote yaliyofanywa na kwamba Ina uzito wa tani tatu ambayo imeonesha miradi mikubwa ya kimkakati ikiwamo ujenzi wa daraja la kigamboni,Reli ya kisasa SGR, Daraja ya John Kijazi, uwanja wa ndege,Ikulu ya Chamwino Dodoma, Ikulu ya Dar es Salaam.
“Mtu anakuja hapa anaona keki ya aina yake yenye uzito wa tani tatu ambayo ina miradi yote mikubwa ambayo Rais Dk Samia amefanya kwa watanzania na inajidhihirisha kwa macho,”; amesema Waziri Kabudi.
Aidha amewapongeza wabunifu wa keki hiyo kutioka Lazziz Bakery Limited huku akisema hata yeye alitamani kuivunja keki hiyo ambapo ameogopa kuharibu maonesho.
Mkurugenzi wa Lazziz Bakery Limited Syed Rizvi amesema keki hiyo ina kilogramu 3000 sawa na uzito wa tani tatu ambayo imetekelezwa kwa kuonesha miradi ya serikali ya awamu ya sita katika kipindi cha miaka minne ya RAIS Dk. Samia.
“Kila mtu anayekuja hapa kuangalia keki hii anafurahi ni keki kubwa Afrika,” ameeleza Mkurugenzi wa Lazziz Bakery.

Awali Mhasibu wa Lazziz Bakery Elizabeth Ligendo amesema keki ilitotengeneza ni ya Kimataifa ambayo imebuniwa kwa kuzingatia miradi mikubwa ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia.