Na Lucy Ngowi
JINA la Suleiman Ikomba ambaye kwa sasa ni Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), si geni katika tasnia ya elimu hapa mchini.
Ikomba amejipambanua kwa moyo wa kujitolea, bidii na uongozi wa kipekee uliojengwa juu ya misingi ya taaluma, utu, na mshikamano.
Safari yake kutoka mwalimu wa kawaida hadi kuwa Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ni simulizi ya uvumilivu, kujituma, na kujitoa kwa ajili ya walimu wa Tanzania.

Akizungumza historia yake anasema kwamba, alianza kazi ya ualimu mwaka 1991 katika Shule ya Msingi Kagongo, Wilaya ya Kigoma.
Kwamba kwa kipindi cha miaka minne alifundisha kama mwalimu wa kawaida, kisha akateuliwa kuwa Mwalimu Mkuu mwaka 1995, ambapo hapo safari yake ya uongozi ilianza rasmi.
Ikomba anasema Mwaka 2001, alihamia Dar es Salaam kusomea ‘Standard Personality Management’ katika Chuo cha Utumishi wa Umma,
Na baada ya hapo akahamishiwa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke.
Katika Manispaa hiyo, aliendelea kuwa Mwalimu Mkuu katika shule mbalimbali ikiwemo Yombo Dovya hapo alifundisha kwa muda mfupi.
Kisha alikwenda shule ya Mtoni 77 iliyokuwa Shule mpya hapo alikuwa Mwalimu Mkuu wa kwanza katika shule hiyo.
Kisha alihamishiwa shule ya msingi Kiburugwa ambapo alikaa kwa wiki mbili tu kutokana na sababu za kiutawala,
Vile vile alihamishiwa Mtoni kwa Mama Mary ilikuwa mwaka 2004 mpaka 2010.

Alifumdisha Minazini mwaka 2010 hadi 2015. Akahamishiwa
Mbaga Rangi Tatu mwaka 2015 hadi 2019. Kisha mwaka 2019 alihamishiwa Shule ya Ali Hassan Mwinyi iliyopo Tandika .
Anasema katika kila shule aliyohudumu, alijenga jina la heshima kwa ufanisi, nidhamu, na moyo wa kuwajali wanafunzi hasa wale waliotoka katika mazingira duni.
Kiongozi wa Walimu: Safari ya Ndani ya CWT
Anasema Mwaka 2006, alichaguliwa kuwa mjumbe wa baraza la wafanyakazi wa manispaa ya Temeke, akiwakilisha walimu.
Hatua ambayo ilifungua mlango wa safari yake ya kikanda ndani ya CWT:
Mwaka 2010 alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Temeke.
Na mwaka 2015 hadi 2020 aligombea ngazi ya mkoa na kuchaguliwa kuwakilisha walimu wa wilaya katika Baraza la Taifa.
Kwamba mwaka 2020 aliteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Taifa ya CWT.
Na mwaka 2023 akachaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa CWT kupitia uchaguzi mkuu uliofanyika Tanga.
Mwaka huu 2025 kwa ridhaa ya mkutano mkuu, akachaguliwa kuwa Rais wa CWT Taifa.
Anaeleza kuwa katika uongozi wake, Ikomba amejitahidi kuunganisha walimu wa Tanzania kupitia usikivu, utetezi wa haki zao, na mawasiliano ya moja kwa moja kati ya chama na serikali.

Anasema mwaka 2023 hadi 2025, akiwa Makamu wa Rais, alishiriki kwenye kampeni ya kitaifa ya “Samia Teachers’ Mobile Clinic”, ambayo ilitembelea karibu mikoa yote, kusikiliza na kutatua kero za walimu moja kwa moja.
Kwa Ikomba, mafanikio ya walimu ni mafanikio ya taifa. Ndoto yake kama Rais wa CWT ni kuona walimu wanapewa heshima wanayostahili, haki zao zinalindwa, na changamoto zao zinapatiwa suluhisho la kudumu.
Anaelezea changamoto zinazoumiza moyo wake kuwa ni kuona Walimu wenye sifa sawa kutopewa madaraja sawa,
Uzembe wa baadhi ya maofisa waliokataa kutekeleza maagizo ya serikali,
Pia uonevu wa wazi unaochangia kuwakatisha tamaa walimu.
Hata hivyo, anasema kwa matumaini kwamba kliniki waliyoendesha imetoa mwanga kwa serikali kutambua ukubwa wa changamoto hizo, na kwamba mabadiliko ya kweli yanawezekana.
Pia Rais huyo wa CWT ana historia ya kugusa maisha ya watoto waliotoka kwenye familia zisizojiweza kwa kuwa alikuwa akiwakusanya wanafunzi waliokosa uwezo wa kulipa ada au vifaa vya shule, na kuwafundisha nyumbani kwake pamoja na mkewe.
Anasema kwamba akiwa na wanafunzi hao aliwapatia chakula na malezi ya kielimu.
Na wengi wao leo ni watu waliotimiza ndoto zao. “Hii ni ushahidi wa mwalimu anayefundisha kwa moyo, si kwa mshahara,”.
Rais Ikomba ni kiongozi wa mfano. Ametoka kwenye ngazi ya chini kabisa ya ualimu hadi kuwa sauti kuu ya walimu Tanzania.
Ndoto yake ni kuwa mtetezi, msimamizi, na mshauri kwa walimu kwa uadilifu, umakini na maono.
Anapoingia kwenye kipindi chake cha uongozi wa 2025 hadi 2030, anaamini kuwa nguvu ya walimu iko katika mshikamano, mafunzo endelevu, na haki za msingi za kiutumishi.
“Chama cha walimu ni cha wanachama na kinapaswa kuzungumza kwa sauti ya walimu wote, si viongozi wachache,” anasema Rais Ikomba.