Na Lucy Ngowi
DODOMA: KATIBU Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha Tanzania inazalisha nguvukazi yenye ujuzi, ubunifu na umahiri unaokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya soko la ajira na maendeleo ya viwanda.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wamiliki wa viwanda, waajiri na wadau wa elimu ya ufundi stadi, Profesa Nombo amesema Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya 2014 (Toleo la 2023) imeweka mkazo katika kujenga mfumo wa elimu unaozingatia ujuzi na tija kwenye soko la ajira.

Amesema kupitia sera hiyo, Serikali imeendelea kuimarisha ubora wa mafunzo, kuongeza ushirikiano kati ya taasisi za elimu na sekta binafsi, na kuhakikisha wananchi wanapata fursa sawa za kujifunza na kujiendeleza.
Kwa mujibu wa Profesa Nombo, VETA ina zaidi ya vyuo 900 vinavyotoa mafunzo kwa zaidi ya wanafunzi 300,000 kwa mwaka, huku Serikali ikiendelea kujenga vyuo vingine 64 ili ifikapo mwaka 2026 kuwe na vyuo 145 kote nchini.
Amesema ushirikiano wa VETA na sekta binafsi umewezesha wanafunzi kupata mafunzo ya vitendo kwenye viwanda, migodi na hoteli, ikiwa ni pamoja na makampuni kama Geita Gold Mining, Barrick na North Mara, jambo linalowawezesha vijana kujifunza kwa vitendo na kujiajiri.
Ameongeza kuwa hadi mwaka 2024 Tanzania ilikuwa na zaidi ya viwanda 8,400, ikiwemo zaidi ya 200 vikubwa, vinavyochangia ajira na pato la Taifa, na kwamba ajira zaidi ya 700,000 zinatarajiwa katika sekta za viwanda, ujenzi na nishati ndani ya miaka mitano ijayo.
Profesa Nombo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya VETA, waajiri na viwanda ili kuhakikisha vijana wanapata ujuzi unaokidhi mahitaji ya uchumi wa viwanda.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Anthony Kasore amesema serikali inawahitaji kuhakikisha elimu ya ufundi stadi inakuwa shirikishi, wanaosoma wakienda kwenye ajira waendane na mahitaji ya soko.
Amesema umuhimu wa wadau ni kuhakikisha VETA inatoa elimu bora, lakini ili kufikia huko wanaanzia kwenye mitaala hivyo ni lazima kukutana nao na kuona namna bora ya kuandaa mitaala hiyo.
“Naomba wadau mbalimbali wa elimu ya ufundi stadi kuendelea kuunga mkono juhudi za kuimarisha kupata mafunzo yanayoendana na soko,” amesema.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Clotilda Ndezi alimwakilisha Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Profesa Sifuni Mchome kwa kusema bodi hiyo inaendelea kutoa msukumo kuhakikisha mafunzo ya ufundi stadi nchini yanakuwa ya vitendo zaidi na yanayoendana na mahitaji ya soko la ajira.

“Bodi imesisitiza katika sera zake na miongozo kuwa mitihani na tathmini za wanafunzi zijikite zaidi kwenye vitendo kuliko nadharia,” amesema.