Na Mwandishi Wetu
IRINGA: MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imeanza kutumia teknolojia ya utambuzi wa visumbufu kwa njia ya vinasaba (DNA) ili kudhibiti uharibifu wa mazao mashambani, katika eneo la Ruaha Mbuyuni, wilayani Kilolo mkoa wa Iringa.
Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea wakulima wa eneo hilo, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru, amesema kwa muda mrefu wakulima wamekuwa wakipoteza mazao yao kutokana na mashambulizi ya magonjwa na wadudu waharibifu, hali ambayo imewaathiri kiuchumi na kijamii.

“Wakulima walikuwa wakitumia viuatilifu bila uhakika wa aina ya visumbufu vinavyoshambulia mimea yao. Hii ilisababisha kutumia dawa zisizo sahihi na kupoteza fedha bila mafanikio,” amesema.
Ameeleza kuwa kwa kutumia teknolojia ya DNA, TPHPA imeweza kutambua aina mbili za bakteria zinazoshambulia zao la vitunguu, na kusababisha mizizi kuoza na mimea kunyauka kabla ya kuvunwa.
“Sasa tumetambua visumbufu husika, na tumeleta viuatilifu vinavyolenga bakteria waliogunduliwa. Hii itasaidia kudhibiti tatizo kwa ufanisi na kuongeza tija kwa wakulima,” amesema.

Kwa upande wake, mkulima, Jane John, amesema ujio wa teknolojia hiyo utasaidia kuongeza uzalishaji, kwani hapo awali mimea ilikuwa ikishambuliwa bila wao kujua chanzo cha tatizo.
“Mboga mboga zilikuwa zikishambuliwa, majani yanakuwa ya njano, hazivutii na hatuwezi kuuza. Lakini sasa tumepata matumaini ya mavuno bora na sokoni tutakuwa na ushindani,” amesema.

Hatua hii ni sehemu ya jitihada za serikali kuhamasisha matumizi ya sayansi na teknolojia katika sekta ya kilimo ili kuongeza uzalishaji na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi pamoja na visumbufu vya mimea.
