DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ameitaka Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), kusomesha watu wengi nje ya nchi kwa kuwa waliopo ni wachache.
Profesa Mkenda amesema hayo leo Februari 19,2025 alipokuwa akizindua Bodi ya TAEC, jijini Dar es Salaam.
“Tulikubaliana kuwapeleka watanzania kwenda kusoma kwenye vyuo bora duniani kwenye mambo ya atomu.
“Watu waliosoma katika atomu wako wachache sana hatuna watu wengi, tunahitaji wawe chuoni kufundisha na tunahitaji kuwa watendaji.
“Tungependa kazi mliyoanza ya kutenga fedha kwa ajili ya mafunzo ya muda mrefu ya vyuo vikuu nje ya nchi kazi hiyo iendeelee,” amesema Mkenda.
Mkenda amesema upo uwezekano mkubwa kwamba mionzi haijatumika kwa ufasaha katika eneo la tiba, kilimo na Kwenye viwanda.
Pia amesema japo kunakuwepo na ufadhili wa masomo, ila haupo kwenye maeneo yanayogusa mionzi, na kuipongeza tume hiyo kwa kutenga bajeti kwa ajili ya kuwapeleka watanzania nje ya nchi kwa ajili ya kujifunza mambo ya mionzi.
“Nawapongeza tume mmetenga bajeti kwa ajili ya kufundisha wa Tanzania nje ya nchi lazima tusisitize twende duniani tukajifunze katika vyuo bora tupeleke watanzania wakasome. Mlisimamie jambo hili kama bodi,” amesema na kuongeza kuwa mtanzania anaposoma vizuri anaisaidia nchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Profesa Najat Kassim Mohammed amesema tume hiyo inatekeleza majukumu ya kudhibiti na kuhamaisha matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia.
Amesema ili kuhakikisha bodi inatekeleza majukumu kwa usahihi kwa kushirikiana na Uongozi Institute wameandaa mafunzo maalum kwa uongozi wa bodi kuanzia Februari 17 hadi 21, 2025.