Na Lucy Ngowi
MKAZI wa Mbezi Luis mkoani Dar es Salaam, Festo Maricha (27) amejeruhiwa na polisi baada ya kutoa panga kwa ajili ya kutaka kumdhuru askari akiwa kwenye majukumu yake ya kikazi.
Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema hayo katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari ya kueleza mikakati ya kuhakikisha usalama wa Jiji la Dar es Salaam unakuwa wa hali ya juu.
Muliro amesema mtuhumiwa Maricha alikuwa na mwenzake ambaye hakufahamika jina alikimbia.
Akielezea tukio hilo amesema, Septemba tatu majira ya saa mbili usiku, jeshi hilo lilipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuwa maeneo ya Kawe Tanganyika Packers, kulikuwa na watu wawili waliokuwa na mapanga.
Amesema watu hao walitishia na kupora wapita njia.
“Ufuatiliaji wa polisi ulifanyika haraka na kuwakuta watu hao ambapo walipotaka kukamatwa walikaidi na kutoa mapanga kutaka kumdhuru mmoja wa askari, ambaye alijihami kwa kupiga risasi hewani.
” Na baadaye alipokuwa kwenye hatari kubwa ya kudhuriwa alimjeruhi kwa risasi mtuhumiwa mmoja Festo Maricha, ambaye amepelekwa hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu,” amesema.