– Uzalishaji wa Asali Wapaa, Uhifadhi Waongeza Mvuto wa Uwekezaji
Na Danson Kaijage
DODOMA: KATIKA kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Mkoa wa Tabora umeonyesha mafanikio makubwa kiuchumi, kijamii na kimazingira, huku pato la mwananchi mmoja likipanda kutoka Sh. Milioni 1.77 mwaka 2020 hadi Sh. Milioni 1.85 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 4.5.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Jijini Dodoma, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paulo Chacha amesema mafanikio hayo ni matokeo ya juhudi za kisekta zilizolenga kuimarisha uzalishaji, kuhifadhi mazingira, na kuvutia uwekezaji.

“Pato la mkoa limeongezeka kutoka Sh. Trilioni 5.4 mwaka 2020 hadi Trilioni 6.3 mwaka 2024. Tabora sasa ni kinara wa maendeleo yanayomgusa mwananchi wa kawaida,” amesema.
Kwa mujibu wa Chacha, uchumi wa mkoa huo umejengwa juu ya kilimo na ufugaji ambavyo huchangia asilimia 70 ya pato la mkoa.
Amesema mazao ya chakula yanayolimwa kwa wingi ni pamoja na mahindi, mpunga, mtama, muhogo, viazi vitamu, uwele na jamii ya mikunde; huku tumbaku, pamba, alizeti, karanga na mchikichi yakiwa ndiyo mazao ya biashara yanayoongoza.
Amesema serikali imetoa zaidi ya Sh. Bilioni 52.8 kwa ajili ya ruzuku ya mbolea, mbegu bora na miradi ya umwagiliaji.
Amesema skimu za umwagiliaji zimeongezeka kutoka 25 mwaka 2020 hadi 46 mwaka 2025, huku eneo la umwagiliaji likipanuka kutoka ekari 16,453.25 hadi ekari 37,560.25.
Kwa upande mwingine amesema mkoa huo ni maarufu kwa uzalishaji wa asali, umeweka historia mpya kwa kufanikisha ujenzi wa viwanda vinne vya kuchakata na kufungasha asali.
Uzalishaji umeongezeka kutoka tani 1,868.6 mwaka 2020 hadi tani 2,002.48 mwaka 2025.
“Mafanikio haya yanatokana na mikakati ya kuwajengea uwezo wafugaji wa nyuki na kuvutia wawekezaji katika sekta hii muhimu,” amesema.
Amesena katika jitihada za kulinda mazingira, misitu ya vijiji imeongezeka kutoka sita mwaka 2020 hadi misitu 37 mwaka 2025, zikiwa na jumla ya ekari 330,780.75 hali iliyochangia kudhibiti uharibifu wa mazingira na kuimarisha vyanzo vya maji, hali inayochochea tija katika kilimo na ufugaji wa nyuki.