Na Mwandishi Wetu
DODOMA:CHUO Kikuu Huria Tanzania (OUT), kinaendesha Mafunzo ya Ufuatiliaji na Tathmini kwa watumishi wa mamlaka za serikali za mitaa pamoja tawala za mikoa ili kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa maendeleo ya miradi inayowekezwa na serikali.
Kaimu Mkurugenzi kitengo cha Ufuatiliaji na Tathimini, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI, Mussa Otieno amesema hayo alipomwakilisha Katibu Mkuu Adolf Ndunguru, wakati akifungua mafunzo ya awamu ya pili ya Ufuatiliaji na Tathmini
Amesema mafunzo hayo yanafanyika ili kuwaimarisha watumishi waliopo katika idara hizo kwani wataimarika katika utendaji wao wa kazi.
Amesema serikali inatumia bajeti kubwa katika mamlaka za serikali za mitaa, hivyo anaamini kuwa baada ya mafunzo hayo watumishi hao watakuwa wameimarika.
“Baada ya mafunzo haya mtumishi atakuwa na uwezo wa kutimiza malengo yanayotakiwa katika masuala ya ufuatiliaji na tathmini ili miradi ya serikali iendane na malengo yaliyopangwa.
“Tukatumie vyema utaalam tutaopata hapa na tukawashirikishe na wenzetu tunaofanya nao kazi pamoja, ili kuwa na timu nzuri kwa ajili ya kuimarisha ufuatiliaji na tathmini katika halmashauri tunazotoka,”amesema.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini wa Utendaji wa serikali, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sakina Mwinyimkuu amesema serikali za mitaa ndiyo mtekelezaji mkubwa wa shughuli za serikali karibia asilimia 70 ya shughuli zote zinatekelezwa na mamlaka ya serikali za mitaa.
Hivyo mafunzo hayo kwa washiriki hao yataiongezea uwezo serikali kufikia malengo yake ya kitaifa ikiwemo dira ya maendeleo.
“Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni mdau anayetusaidia kujengea uwezo taasisi za umma katika ufuatiliaji na tathmini, serikali za mitaa ndiyo watekelezaji wa shughuli za serikali na ndiyo wanaotoa picha ya utendaji wa serikali kwa jamii.
“Hili ni eneo linaloweza kuwabadilisha mitizamo ya wananchi na kuwajengea imani kwa serikali yao kwa kuona inasimamia vyema utekelezaji wa sera, miradi na mipango.
‘Hivyo mafunzo haya yatawasidia vyema utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoibuliwa na halmashauri na mingine ya kitaifa inayotekelezwa katika halmashauri,” amesema.
Mratibu wa Mafunzo ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi kutoka OUT, Dkt. Emmanuel Mallya amesema chuo hicho kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, kinaendesha mafunzo hayo ili serikali iweze kushuhudia mabadiliko makubwa ambayo yanalenga kuimarisha utendajikazi hasa katika upande wa ufuatiliaji na tathmini.
Mwenyekiti wa washiriki wa mafunzo hayo ambaye ni Katibu Tawala msaidizi sehemu ya Usimamizi, Ufutiliaji na Ukaguzi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Pius Ngaiza, ameishukuru serikali kwa kuwapa mafunzo hayo kwa kuwa wengi walikuwa wanafanya tathmini na ufuatiliaji katika namna ambayo ilileta shida hasa katika ukaguzi,.
Amesema mafunzo hayo yamewaimarisha hivyo watafanya kazi kwa kufuata mfumo unaotakiwa kiofisi na hata kitaifa.
Mafunzo haya ni mwendelezo wa mafunzo ya awali yaliyoendeshwa katika jiji la Arusha kanzia Oktoba saba hadi 11, 2024.
Wasiriki 90 kutoka mikoa 13 walishiriki ambapo kiujumla inakuwa asilimia 70 ya halmashauri, manispaa na majiji yote nchini kupata mafunzo hayo ya ufuatiliaji na tathmini.