Na Mwandishi Wetu
CHUO Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kimeunda Kamati ya Ufuatiliaji na Tathmini itakayosimamia na kufuatilia tathmini ya utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), chuoni hapo.
Katika uzinduzi huo, Mratibu Msaidizi wa Kitaifa wa Mradi wa HEET, Dkt. Evaristo Mtitu amesema kamati hiyo itatakiwa kuandaa ripoti zote zinazohusiana na utekelezaji wa mradi huo.

Amesema ripoti hizo ndizo zitakazokaguliwa na mamlaka mbalimbali zilizoidhinishwa kufanya hivyo pamoja na wafadhili wa mradi ambao ni Benki ya Dunia.
“Huu ni mradi wa kimkakati hivyo malengo mliyojiwekea ambayo yalikubaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Benki ya Dunia mnatakiwa kuyaangalia yatimizwe kwa uadilifu, Kamati hii ni jicho la utekelezaji wa huu mradi, hii ni dhamana kubwa sana mliyopewa,” amesema.
Makamu Mkuu wa chuo hicho Profesa Elifas Bisanda, amesema kamati hiyo ni muhimu katika kipindi hiki OUT kinafanya utekelezaji wa Mradi wa HEET katika kipindi ambacho ujenzi wa majengo ya maabara unaanza kwenye kanda saba.

“Huu mradi ni wetu, tumekuwa tukipata changamoto na gharama kubwa tunapofika kwenye suala la matumizi ya maabara,
“Mradi wa HEET unakwenda kutatua tatizo hilo hivyo kamati hii ikasimame vyema na imara kuhakikisha hakuna kinachoharibika kwa namna yoyote ile kwa kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa kufuata matakwa ya mradi,” amesema.
Akizungumza katika uzinduzi huo Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Tafiti na Huduma za Kitaalam na Mratibu wa Mradi wa HEET chuoni, Profesa Alex Makulilo, amesema baada ya uzinduzi huo, kamati itahakikisha usimamizi na ufuatiliaji wa mradi unaimarika.
HEET unatekelezwa na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kupitia udhamini wa Benki ya Dunia unaolenga kuimarisha taasisi za elimu ya juu katika maeneo ya miundombinu, ufundishaji na ujifunzaji ambapo Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimepata takribani Dola Milioni tisa.