Na Mwandishi Wetu
TABORA: HALMASHAURI ya Mji wa Nzega inatarajia kuanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kilomita 10.6 za barabara za lami katika maeneo ya pembezoni na nje ya mji.
Kaimu Mkurugenzi wa Mji wa Nzega, Ajalii Malimwengu, amesema miradi hiyo ni sehemu ya juhudi za Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini, Hussein Bashe, za kuvutia ufadhili kutoka kwenye mradi wa Kuboresha Miundombinu Mijini (TACTC) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Amesema mradi huo unalenga kuboresha usafiri wa watu na bidhaa, kuimarisha usalama, na kuinua hadhi ya mji huo.

Pia amesema Nzega itapata Soko Kuu la kisasa litakalojengwa kwa ajili ya wafanyabiashara, hatua inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa biashara na kuongeza kipato cha wafanyabiashara, hivyo kuchangia uchumi wa mji huo.
“Leo tunapitia matokeo ya tathmini kutoka kwa mshauri mwelekezi kabla ya hatua nyingine muhimu kufuata ,” amesema.
Ametaja barabara zitakazojengwa kuwa ni Barabara ya Ferouz, Swahili–Kachoma, Kalangale Moja na Mbili, pamoja na Barabara ya Dkt. Massam–Chief Ntinginya.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya GaugePro Consult Limited, ameeleza baada ya kufanya ziara ya eneo la mradi, changamoto mbalimbali zimebainika.
Ametaja changamoto hizo ni pamoja na uwepo wa mabomba ya maji, nguzo za umeme, na miti katika maeneo yanayotarajiwa kujengwa.
Amesema ushauri utatolewa kuhusu namna ya kushughulikia changamoto hizo na athari zake za kifedha.
Mshauri kutoka Benki ya Dunia, Dkt. Alphonce Tiba, amesisitiza umuhimu wa kushughulikia masuala ya mazingira na tamaduni ili kuhakikisha mradi unakidhi mahitaji ya jamii.
“Hakikisheni mnashirikisha wadau wote muhimu na kujumuisha maoni yao katika upangaji wa miradi.
Kwa mfano, ujenzi wa soko kuu utawaathiri wafanyabiashara 350 wa sekta sita tofauti, hivyo ni muhimu kufahamu matarajio yao,” Dkt. Tiba amesema.
Kwa upande wake, Kondwanie Chirembo, Mtaalamu Mwandamizi wa Usimamizi wa Hatari za Majanga kutoka Benki ya Dunia, amesisitiza umuhimu wa kufanya uchunguzi wa kina wa udongo ili kuhakikisha uimara wa miradi na kuepuka nyufa katika miundombinu.
Amesema ripoti ya mradi inapaswa kuwa na taarifa wazi juu ya jinsi barabara zitakavyounganishwa na namna zitakavyojengwa ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.