Na Mwandishi Wetu
GEITA: SHIRIKA la Bima la Taifa (NIC) linaendelea kutoa elimu na huduma mbalimbali za bima kwa wananchi kupitia Kijiji cha Bima, kilichopo katika Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.
Ofisa Uhusiano Ephrasia Mawala amesema hayo katika maonesho ya madini mkoani Geita.
Amesema maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kutoa elimu ya kifedha kwa wananchi, hasa kuhusu bima kama nyenzo ya kujikinga na athari za kiuchumi zinazotokana na majanga mbalimbali kama moto, ajali, maafa ya asili na mengineyo.
Amewakaribisha wananchi kutembelea banda la Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) katika Kijiji cha Bima, ili kupata huduma na maelezo kutoka kwa NIC pamoja na watoa huduma wengine wa bima waliopo katika eneo hilo.
Amesema Kijiji cha Bima ni mkusanyiko wa watoa huduma za bima kutoka kampuni mbalimbali nchini, unaoratibiwa na TIRA kwa lengo la kuwawezesha wananchi na wadau wa sekta ya madini na biashara kupata elimu, ushauri na huduma za bima kwa karibu.
Amesema NIC ikiwa ni shirika la umma linalotoa huduma za bima nchini, inashiriki kikamilifu kwa kutoa huduma za bima ya maisha, bima ya mali, bima kwa wachimbaji, pamoja na ushauri wa kitaalamu kuhusu aina sahihi za bima kulingana na mazingira ya kijamii na kibiashara.