Na Lucy Ngowi
BEI ya bidhaa muhimu za vyakula zimeendelea kupanda nchini, huku mfumuko wa bei wa Taifa ukifikia asilimia 3.4 kwa mwaka ulioishia Agosti 2025, ukilinganishwa na asilimia 3.3 mwezi Julai mwaka huo.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), bidhaa zilizochangia kwa kiasi kikubwa ongezeko hilo ni pamoja na mchele, ambao bei yake imepanda kutoka asilimia 7.8 hadi asilimia 10.5, mtama kutoka asilimia 2.1 hadi 5.5, na unga wa mtama kutoka asilimia 6.1 hadi 10.2.

Aidha, ndizi mbichi za kupikwa zimeonesha ongezeko kubwa zaidi kutoka asilimia 2.7 hadi asilimia 12.0. Mikate nayo imepanda kutoka asilimia 18.8 hadi 19.3, kuku wa kienyeji kutoka asilimia 12.1 hadi 17.1, mayai ya kuku kutoka asilimia 3.9 hadi 6.4, na mafuta ya kupikia kutoka asilimia 5.8 hadi 6.9.
Vilevile, matunda yamepanda kutoka asilimia 3.6 hadi 5.2, huku bei za vinywaji visivyo na kilevi kama juisi na soda zikiongezeka kutoka asilimia 3.3 hadi 3.5.
Kwa upande wa bidhaa zisizo za chakula, taarifa ya NBS inaonesha kuwa sigara zimepanda kutoka asilimia 5.8 hadi 6.0, viatu vya wanawake kutoka asilimia 1.0 hadi 1.6, na viatu vya watoto kutoka asilimia 1.8 hadi 2.2.
Bidhaa za matumizi ya nyumbani pia zimeathirika. Bei ya vitanda imepanda kutoka asilimia 2.2 hadi 3.3, jokofu kutoka asilimia 0.4 hadi 1.5, jiko la umeme kutoka asilimia 1.7 hadi 2.0, na jiko la mkaa kutoka asilimia 7.3 hadi 11.4.
Bei ya vyombo kama sahani imeongezeka kutoka asilimia 3.5 hadi 5.0, vikombe kutoka asilimia 1.9 hadi 2.5, na dawa ya mbu kutoka asilimia 8.5 hadi 9.0.
Kwa upande wa usafiri na teknolojia, pikipiki zimepanda kutoka asilimia 2.7 hadi 3.5, simu za mkononi kutoka asilimia 0.2 hadi 1.5, na kompyuta mpakato kutoka asilimia 3.0 hadi 5.2.
Aidha, bidhaa na huduma zinazohusiana na starehe, michezo na utamaduni nazo zimeonesha ongezeko kutoka asilimia 1.0 hadi 1.4.
Kwa ujumla, mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi umeongezeka hadi asilimia 7.7 kwa mwaka ulioishia Agosti 2025, kutoka asilimia 7.6 mwezi Julai. Vilevile, mfumuko wa bei wa bidhaa zisizo za chakula umeongezeka hadi asilimia 1.6 kutoka 1.5 kwa kipindi kama hicho.
Katika ukanda wa Afrika Mashariki, hali ya mfumuko wa bei imeonesha tofauti. Nchini Uganda, kiwango kimesalia asilimia 3.8 kama kilivyokuwa mwezi Julai, huku nchini Kenya, mfumuko wa bei umeongezeka kutoka asilimia 4.1 hadi 4.5 kwa mwaka ulioishia mwezi huo.