Na Danson Kaijage
DODOMA: CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimesema kuwa kitashiriki Uchaguzi Mkuu wa 2025 wa kuwachagua madiwani, wabunge na Rais, hakitaungana na chama chochote kupinga au kugomea uchaguzi huo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Joseph Selasini amesema hayo alipozungumza katika Mkutano Mkuu wa kikatiba wa chama hicho uliofanyika mkoani Dodoma.
Selasini amesema chama hicho hakiko tayari kususia uchaguzi kwani kinafuata matakwa ya kikatiba ya kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano ya kikatiba.
Amesema hakijaungana na vyama vingine kupinga uchaguzi kwa kuwa hawana elimu ya kitosha juu ya wanachokiamini kupitia kaulimbiu ya ‘No Roform No Election’.
Sababu nyingine amesema ni vyama vingine kukidharau chama hicho kwa maelezo ni kidogo.
Selasini amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha kauli mbiu ya “Kazi na Utu” kwa maelezo kuwa NCCR–Mageuzi imekuwa ikihamasisha zaidi kwa kutumia kauli mbiu ya “Utu Itikadi yetu”.
Kwa upande wake Msajili msaidizi wa vyama vya siasa Nchini Disty Nyahoza amesema vyama vya siasa vipo kwa ajili ya kuhakikisha vinajenga hoja na kutaka kushika dola lakini siyo vurugu.
Naye Mwenyekiti wa Chama hicho Haji Ambar Khamis amesema chama kinafanya mkutano wake kikatiba na kuhakikisha kinapata viongozi kama sheria ya vyama vya siasa inavyotaka.