Na Lucy Ngowi
GEITA: MWENYEKITI wa Chemba ya Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Geita, Robert Gabriel ameeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya viwanda, hasa viwanda vya bidhaa za ngozi na nyama nchini Tanzania.
Gabriel ameelezea mafanikio hayo alipozungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya nane ya Sekta ya Madini mkoani Geita.
Amesema uwepo wa viwanda hivyo unathibitisha kuwa Tanzania ya viwanda si ndoto tena bali ni uhalisia unaoonekana.

Ametoa mfano wa kiwanda cha zamani cha viatu cha Bora, kilichokuwa maarufu enzi za Mwalimu Nyerere, akisema sasa bidhaa zake zimehuishwa kupitia kiwanda cha Kilimanjaro International Leather Industries, kinachozalisha viatu vya ngozi kutoka kwa wanyama walioko nchini Tanzania.
“Leo hii, viatu vya Kilimanjaro Leather ni vya ubora wa kimataifa. Ni imara na vinafaa kwa wanafunzi wa kike na wa kiume. Wazazi wanaojali watoto wao wanapaswa kuvitumia,” amesema Mwenyekiti huyo.

Ametoa wito kwa wafanyabiashara nchini kuacha kuagiza viatu kutoka nje ya nchi na badala yake watangaze na kuuza bidhaa za ndani ili kusaidia kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuchangia mapato ya kodi kwa serikali.
Aidha, ameelezea mafanikio ya kiwanda cha kuchakata nyama kinachomilikiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), kwamba kiwanda hicho hufuga ng’ombe, huchinja, na kusindika nyama kwa viwango vya kimataifa.
Amesema tayari bidhaa zake zina soko katika nchi mbalimbali zikiwemo Qatar, Saudi Arabia, na mataifa mengine.

“Tumezoea kula nyama ngumu kwa sababu ya kuchinja wanyama waliodhoofika. Leo hii, Tanzania tuna nyama laini na bora inayozalishwa hapa hapa nchini kwa kiwango cha kimataifa,” amesema.
Akizungumza kwa niaba ya kiwanda cha Kilimanjaro International Leather, Ofisa Mauzo Mwandamizi, Christopher Manyani, amesema bidhaa zao zina ubora wa hali ya juu huku bei zake zikiwa nafuu, kulingana na aina ya viatu.
Amesisitiza kuwa Watanzania wanapaswa kuachana na dhana ya kudhani bidhaa kutoka nje ni bora zaidi.
Kwa upande wake, Noel Tuga, Ofisa Mwandamizi wa Uwekezaji kutoka PSSSF, amesema mfuko huo unaendelea kusimamia kwa karibu miradi ya wanyama na viatu, akisisitiza kuwa viwanda hivyo vina mchango mkubwa katika kuinua uchumi na kuongeza ajira.
Katika maonesho hayo, Chemba ya Wafanyabiashara ilitoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuyawezesha maonesho hayo kufanyika kila mwaka na kwa kuhakikisha maboresho katika sekta ya madini na viwanda yanatekelezwa kwa vitendo.
Mwenyekiti wa Chemba Gabriel amesema, agizo la Rais kuhusu maboresho ya miundombinu limeleta mafanikio makubwa, yakiwemo majengo ya kudumu kwa taasisi mbalimbali, ikiwemo Wizara ya Madini na PSSSF.
Aidha, amesema maonesho hayo yamevutia wageni kutoka nchi za jirani kama Rwanda, Burundi, Sudan ya Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na Kenya, ambao wanashiriki kwa ajili ya fursa za biashara.
“Kama Chemba, tunahakikisha tunakuwa sauti ya makundi yote haya. Tutaendelea kushirikiana na serikali na wadau wengine kuhakikisha mafanikio haya yanaendelezwa,” amesena.