Na Mwandishi Wetu
MGOMBEA wa urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalim, ameahidi kuirejeshea Jiji la Dar es Salaam hadhi yake ya awali endapo atachaguliwa kuwa Rais.
Akihutubia wakazi wa Dar es Salaam katika moja ya mikutano ya kampeni, Mwalim amesema kuwa Dar es Salaam ni kitovu cha biashara na uchumi nchini, hivyo inastahili kuwa na Meya wa Jiji mwenye mamlaka kamili ya kisheria na kiutendaji.
“Nitairudishia Dar es Salaam heshima yake ya kuwa Jiji kamili, lenye Meya wa kuchaguliwa atakayewajibika kwa wananchi. Jiji hili linaingiza mapato makubwa serikalini, hivyo linastahili kuheshimiwa,” amesema.

Pamoja na hilo, ameeeleza dhamira yake ya kuboresha maisha ya watumishi wa umma kwa kuongeza kima cha chini cha mshahara hadi Sh. Milioni nane ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuinua uchumi wa familia na kupunguza utegemezi.
“Naombeni mniamini na kunipa nafasi hii. Nina nia ya kweli ya kubadili maisha ya Watanzania. Vijana wapate ajira stahiki — maana kubeti si kazi,” amesema.
Katika mkutano huo huo, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kinondoni kupitia CHAUMMA, Moza Ally, amewataka wananchi wa jimbo hilo kumchagua kwa msingi wa utendaji usio na ubaguzi.
“Baada ya kuapishwa, sitakuwa mbunge wa mfukoni. Nitakuwa mbunge wa wananchi wote. Wale waliokata tamaa waamini tena kuwa kuna matumaini,” amesema.
Moza ameahidi kuwa ofisi ya mbunge itakuwa wazi kwa wananchi wa vyama vyote na kusimamia upatikanaji wa mikopo ya maendeleo, hususani kwa vijana na wanawake, ambayo amedai kwa muda mrefu imekuwa changamoto.
“Kila mwananchi atahudumiwa bila kujali itikadi ya kisiasa. Ile mikopo mliyokuwa mkiikosa, sasa mtaipata,” amesema.
Wagombea hao wamekuwa wakihimiza siasa za heshima na kujikita katika sera zenye kuangazia maendeleo na ustawi wa wananchi, wakitumia kaulimbiu ya mabadiliko ya kweli.