Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM: MGOMBEA urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalim, amesema akichaguliwa kuongoza nchi, atamteua mgombea ubunge wa Jimbo la Kivule, Benson Kigaila, kuwa Waziri Mkuu.
Akizungumza na wananchi wa Kivule, Mwalim amesema Kigaila anatosha kushika wadhifa huo.
“CCM biashara imeisha… nendeni na Kigaila, nichagulieni kaka yangu, pacha wangu wa kisiasa — ndiye atakuwa Waziri Mkuu wangu,” amesema Mwalim.

Amesema ameamua kuweka wazi siri hiyo kwa kuwa Kigaila anaijua nchi vizuri na amezunguka maeneo mengi.
“Kigaila ni mzee wa field, ndiye atakayekwenda kutatua changamoto zilizosababishwa na CCM,” ameongeza.
Mwalim amewasisitiza wananchi kumchagua Kigaila ili aende akachangamshe Bunge kwa hoja zenye weledi.
Aidha, alisema CHAUMMA imejipanga kutatua matatizo yanayowakabili wananchi wa Dar es Salaam ikiwemo michango katika shule za serikali, huduma kwa akina mama wajawazito, mikopo ya wajasiriamali na ajira kwa vijana.

“Hakuna wazo la kibiashara la Mtanzania litakalokufa. Serikali yangu itawekeza kwenye taasisi za kifedha ili kufanya mapinduzi ya kiuchumi,” alisema.
Ameongeza kuwa serikali yake itapambana na changamoto za kilimo na ajira, akisisitiza kuwa tatizo hilo linapaswa kushughulikiwa kwa umoja na si kwa misingi ya vyama.