Na Mwandishi Wetu
MOROGORO: CHAMA cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimesema maendeleo ya watu yanategemea umakini na uadilifu katika usimamizi wa rasilimali ambazo taifa limejaaliwa na Mwenyezi Mungu.
Mgombea urais wa CHAUMMA, Salum Mwalim, amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zilizojaaliwa kila aina ya rasilimali.
“Kila kona ya nchi hii kuna dhahabu, almasi, tanzanite, madini ya kutengeneza ndege, rubi na makaa ya mawe,” amesema.

Ameeleza kuwa licha ya utajiri huo, wananchi wanaendelea kuishi katika umaskini uliosababishwa na uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Mungu ametupa ardhi kubwa nzuri kwa ajili ya kilimo na mifugo… ni nini utakachotaja hakipo? Lakini bado tuna umaskini. Hii ni kwa sababu ya CCM,” amesema.
Akizungumzia gharama kubwa za chakula, amesema suluhisho ni kuongeza uzalishaji na kupunguza bei za bidhaa sokoni.
“Kupanga ni kuchagua. Mimi nimechagua kilimo kwa sababu ardhi tuliyonayo si ya kuipigia magoti kwa Mchina wala Mmarekani,” amesema na kuongeza:
“Tuna mamilioni ya hekari za kulima miwa, tuna mbegu na tuna nguvu kazi ya kutosha, lakini kila mwaka tuna tatizo la sukari… hizo ndizo akili za CCM.”