Na Mwandishi Wetu
DODOMA: BUNGE limepitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Kazi Na. 13 wa Mwaka 2024 ambao umeongeza likizo ya uzazi kwa wanaojifungua watoto njiti.
Akiwasilisha maelezo ya muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Kazi wa Mwaka 2024, Waziri Antony Mavunde alisema hayo alipomwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete.
Kwa mujibu wa Muswada huo. Mwajiriwa ambaye atajifungua mtoto njiti, ataongezewa muda wa likizo ya uzazi ambao utajumuisha ule uliobaki kufikia wiki 40 za ujauzito.
Hilo likifanyika kwa mama, serikali imeridhia baba wa mtoto huyo njiti kupewa siku saba za mapumziko, kutoka siku tatu za awali.
Hoja hiyo ya kuongezewa likizo ya uzazi kwa wanaojifungua watoto njiti, imekuwa ikizungumziwa kwa muda mrefu na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania ( TUCTA), kwa lengo la kulinda ustawi na afya za watoto wanaozaliwa kabla ya wakati ambao wanahitaji muda wa kutosha wa uangalizi wa mama.
Mavunde pia amesema kifungu kipya cha 34A kinapendekezwa kuongezwa ili kumwezesha mwajiri kumpatia mwajiriwa likizo bila malipo isiyozidi siku 30 ili kuweka mazingira mazuri yatakayomwezesha mwajiriwa kupata likizo bila malipo kutokana na majanga au dharura zinazoweza kujitokeza.
Pamoja na hayo, kifungu cha 14 kinapendekezwa kubainisha aina ya mikataba ya muda maalum ili kuongeza wigo wa mazingira ambayo mtu anaweza kuajiriwa kwa mkataba wa kipindi maalum, ikiwamo mikataba ambayo mwajiriwa anaajiriwa kwa muda ili kuendana na ongezeko la wingi wa kazi, kutoa fursa kwa wahitimu wa vyuo ili kuwajengea uwezo na kufanya kazi nyingine za misimu.
vile vile amesema mwajiri na mwajiriwa wanaweza kuingia katika makubaliano ya namna watakavyofanya kazi katika hali ya dharura inayoweza kuathiri uzalishaji mahali pa kazi wakati wa magonjwa ya milipuko na matukio ya dharura.
amesema kifungu cha 37 kimeweka masharti yanayozuia mwajiri kutoanzisha au kuendelea na shauri la nidhamu dhidi ya mwajiriwa pale ambapo mgogoro huo upo mbele ya Tume au Mahakama ya Kazi ili kuzuia uingiliaji wa mchakato kushughulikia migogoro.
Katika muswada huo amesema fidia zimeainishwa kulingana na aina ya mgogoro na kuweka ukomo wa chini na wa juu wa fidia inayotolewa kwa mwajiriwa aliyeachishwa kazi isivyo halali huku Kifungu cha 41A kinapendekezwa kuongezwa ili kuweka masharti kuhusu afua kwa uvunjaji wa mkataba wa ajira ya muda maalumu.
“Kifungu cha 71 kimeweka masharti ya utaratibu wa kuanza kutumika kwa mikataba ya hali bora inayoingiwa na wakuu wa taasisi za umma. Lengo la marekebisho haya ni kuwianisha masharti ya sheria hii na utaratibu uliowekwa kwenye sheria zinazosimamia utumishi wa umma,” amesema.
amefafanua kwamba vyama vya wafanyakazi vimewezeshwa kwa pamoja kuingia mikataba ya hali bora na mwajiri au vyama vya waajiri kwa ajili ya kuanzisha majukwaa ya ushiriki wa waajiriwa mahali pa kazi.
maelezo yake ni kwamba kifungu cha 94 kimeweka masharti ya kuzuia wahusika wa mgogoro kuwasilisha maombi ya mapitio kwa maamuzi madogo ya Tume isipokuwa kama maamuzi hayo yana athari ya kumaliza mgogoro.
Akisoma maoni ya Kamati Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Fatuma Toufiq ameshauri serikali kuona namna ya kufanya maboresho katika sheria ili kuruhusu pia wanaojifungua watoto wenye mahitaji maalum kama vile usonji, vichwa vikubwa, mgongo wazi, mdomo sungura, matundu kwenye moyo, seli mundu ili kupewa likizo maalum ya uzazi pindi wanapojifungua.